NEWS

Thursday 22 April 2021

Chui anavyothaminiwa Tarime Vijijini

Chui

WAKAZI wa vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa wilaya ya Tarime mkoani Mara, wamehimizwa kuthamini wanyamapori wote kama wanavyomthamini chui.

 

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard katika mkutano na wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Masanga na baadaye kwenye mkutano wa hadhara wa wanakijiji, leo Aprili 22, 2021.

 

Wakazi wa kijiji hicho na vingine vilivyopo katika tarafa ya Ingwe kidesturi wanajiitia jina la mnyama chui (kwa kabika la Wakurya anaitwa Ingwe), hivyo wanamheshimu na kumthamini mnyamapori huyo kiasi kwamba hawathubutu kumuua.

 

"Ninyi huku mnaheshimu chui, vivyo hivyo kuna watu wengine wanajiitia na kuheshimu wanyama wengine kama simba, nyumbu, tembo na kadhalika, hivyo basi mheshimu pia wanyama wote kwani wanyama wahahitaji kuishi kama binadamu tunavyohitaji kuishi," amesema Hobokela.

Mhifadhi Hobokela (kulia) akiwasilisha mada katika mkutano wa hadhara wa wakazi wa kijiji cha Masanga.
 

Aidha, Mhifadhi huyo amewakumbusha wananchi hao kuepuka makosa ya ujangili yakiwemo ya uwindaji haramu wa wanyamapori, kulisha mifugo na kukata miti ndani ya hifadhi.

 

Amesema Idara ya Ujirani Mwema ni kiunganishi cha Hifadhi na jamii katika kujenga na kuboresha uhusiano mwema ikiwa ni pamoja na kuwezesha wananchi kunufaika na miradi ya kijamii kutokana na sehemu ya mapato ya utalii.

 

"Lakini pia, kutokana na changamoto ya kipato duni kwa wananchi, Hifadhi sasa imejielekeza katika kuwezesha miradi ya kiuchumi ambayo ni rafiki kwa mazingira - inayoibuliwa na wananchi wenyewe kupitia vikundi," ameongeza Hobokela.

 

Amefafanua kuwa Hifadhi inachangia asilimia 90 na wananchi wanachangia asilimia 10 katika utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba kwenye hiyo asilimia 10, wananchi wanaweza kuchangia mawe, mchanga, kokoto, n.k.

Baadhi ya akina mama waliohudhuria mkutano huo wakifuatilia mada kutoka kwa Mhifadhi (hayupo pichani).
 

Kwa mujibu wa Hobokela, lengo la jitihada hizo za Hifadhi ya Taifa ya Serengeti chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni kuongeza mnyororo wa thamani kwa wananchi na hivyo kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori katika maeneo husika.

 

Kwa upande wao, wananchi hao wamepongeza Hifadhi hiyo kwa kuandaa mikutano ya kuboresha uhusiano na ujirani mwema, na wameiomba kutekeleza kwa vitendo mipango ya kuwasaidia katika utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi.

 

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia Idara yake ya Ujirani Mwema inaendelea na ziara ya kukutana na viongozi na wakazi wa vijiji 10 vilivyo jirani na hifadhi hiyo upande wa wilaya ya Tarime kwa ajili ya majadiliano ya kuboresha uhusiano na kukubaliana namna bora ya kushirikiana katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori na Mazingira.

 

Vijiji hivyo ni Kitawasi, Masurura, Masanga, Nyabilongo, Kenyamosabi, Karakatonga, Gibaso, Nyandage, Mangucha na Kegonga.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages