NEWS

Tuesday, 27 January 2026

Wizara ya Maji yaandaa mikutano mikuu mitatu ya kitaifa




Na Mwandishi Wetu

Wizara ya Maji imeandaa mikutano mikuu mitatu ya sekta ya maji itakayofanyika jijini Dodoma kuanzia leo Januari 27 hadi 30, 2026.

Mikutano hiyo ni Mkutano wa Mwaka wa Tisa wa Bodi za Maji za Mabonde, Mkutano wa Saba wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Uzinduzi wa Bodi ya Tano ya Taifa ya Maji.

Kaulimbiu ya mikutano hiyo ni “Uhakika wa Maji kwa Maendeleo ya Taifa: Utekelezaji wa Dira 2050 katika Ustahimilivu, Usawa na Uendelevu.”

“Kaulimbiu hii inalenga kuhimiza uwekezaji na juhudi za pamoja katika kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali za maji kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa.

“Mikutano hii ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji kupitia mageuzi ya miaka zaidi ya 25, ikiwemo utekelezaji wa Mipango Jumuishi ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji (IWRMD) chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP).

“Mageuzi hayo yamelenga matumizi endelevu ya maji, ulinzi wa vyanzo vya maji, na kuongeza uwezo wa taifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji.

Mikutano hiyo pia inalenga kuoanisha mipango ya sekta ya maji na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayotambua rasilimali za maji kama mhimili wa ustahimilivu wa taifa, maendeleo ya viwanda, kilimo chenye tija, nishati, uchumi wa buluu na kijani, pamoja na ujenzi wa taasisi imara zenye uwajibikaji.

Mkutano Mkuu wa Tisa wa Bodi za Maji za Mabonde utatoa fursa ya kutathmini utendaji wa bodi hizo kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, kubaini mafanikio na changamoto, na kuweka mwelekeo wa kimkakati kwa kipindi kijacho, hususan kuelekea kukamilika kwa utekelezaji wa WSDP, Juni 2026.

Aidha, Mkutano wa Saba wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka utaangazia mikakati ya kuimarisha uhakika wa maji kwa kushirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwemo mazingira, afya, kilimo, nishati na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wizara ya Maji inakaribisha vyombo vya habari, wadau wa sekta ya maji, washirika wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wengine kushiriki na kufuatilia mikutano hiyo muhimu kwa mustakabali endelevu wa usimamizi wa rasilimali za maji nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages