NEWS

Sunday 25 April 2021

Mwekezaji atoa bilioni moja kujenga kanisa Serengeti, wanakijiji wafurahia matunda ya uwekezaji

Sehemu ya ujenzi wa Kanisa Katoliki unaofadhiliwa na mwekezaji wa Kampuni ya Grumeti Reserves katika kijiji cha Natta-Mbiso

MWEKEZAJI wa Kampuni ya Grumeti Reserves ametoa Dola za Kimarekani 450,000 (sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni moja) kugharimia ujenzi wa Kanisa Katoliki la kisasa katika Kijiji cha Natta-Mbiso wilayani Serengeti, Mara.

 

“Mwekezaji wetu ni muumini wa Kanisa Katoli na mara nyingi anapokuwa hapa anashiriki ibada katika kanisa hilo la kijiji cha Natta-Mbiso, hata wafanyakazi wetu wengi wanasali pale.

 

“Ameona umuhimu wa kuweka hiyo alama kutokana na uhusiano wa muda mrefu alionao na kanisa hilo pamoja na wanakijiji, na fedha hizo alizotoa ni direct contribution (mchango wa moja kwa moja) kwa kanisa hilo.

 

“Kanisa liliomba msaada wa kumalizia uezekaji wa paa la jengo lililokuwa likitumika, lakini tulipofika na kufanya tathmini tuliona kuna mahitaji ya kujenga kanisa zima badala ya paa pekee,” Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu (HR) wa Kampuni ya Grumeti Reserves, Martha Lukumay Baare ameiambia Mara Online News, hivi karibuni.

 

Martha amebainisha kuwa kanisa hilo linajengwa na kampuni dada ya Grumeti Reserves inayojulikana kama Grumeti Construction kwa kuwatumia wataalamu bobezi wa ujenzi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

 

Amesema ujenzi wa kanisa hilo ulianza Aprili 24, mwaka huu na utakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita, ukihusisha pia ujenzi wa choo na matengenezo au ununuzi ya mabenchi ya kisasa ya kukalia.

Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu (HR) wa Kampuni ya Grumeti Reserves, Martha Lukumay Baare
 

Akizungumzia msaada huo, Katekista wa Kanisa Katoliki Kigango cha Natta-Mbiso, Elias Nyakiboha amemshukuru mwekezaji wa Kampuni ya Grumeti Reserves kukubali kuwajengea kanisa la kisasa akisema litasaidia kuwajenga watu kiimani.

 

“Kwa ujumla mwekezaji huyu amebeba ujenzi wote wa kanisa hili… litakuwa kanisa lenye uwezo wa kuhudumia watu 600 kwa wakati mmoja. Haya ni matunda ya uhifadhi, tutatumia kanisa hili la kisasa pia kufundisha waumini wetu kuthamini uhifadhi na utunzaji wa mazingira,” amesema Nyakiboha.

 

Kwa upande wake, Deogratias Mganga ambaye ni kiongozi wa kanisa hilo na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Saerikali ya Kijiji cha Natta-Mbiso, amesema “Huu [ujenzi wa kanisa hilo] ni mradi mkubwa na wa gharama kubwa kuliko mingine yote tuliyokwishapata katika kijiji chetu kwa ufadhili wa mwekezaji huyu.”

 

Naye kiongozi mwingine wa kanisa hilo, Rose Nyambura amesema “Ujenzi wa kanisa hili ukikamilika tutapata sehemu nzuri sana ya kusali. Jengo lililokuwepo lilikuwa limechakaa, tulikuwa tunapata shida wakati wa kusali, wakati mwingine tukinyeshewa mvua na kuchomwa jua.”

 

Kampuni ya Grumeti Reserves imewekeza katika shughuli za kitalii na uhifadhi huku ikiendesha hoteli kadhaa za kifahari ikiwemo Sasakwa wilayani Serengeti.

 

“Mbali na mradi huu wa kanisa, kampuni ya Grumeti Reserves pia imekuwa ikisaidia utekelezaji wa miradi ya kijamii katika vijiji 22 vilivyopo ndani ya wilaya za Serengeti na Bunda mkoani Mara,” amesema Martha.

 

Misaada ya kijamii na ajira zinazotolewa na mwekezaji huyo kutoka nchi ya Marekani, imesaidia kuwafanya wakazi wa vijiji hivyo kutambua umuhimu wa uhifadhi, hivyo kuunga mkono juhudi za uhifadhi wanyamapori.

 

Viongoji wa kijamii wanamtaja mwekezaji huyo kama kielelezo na mfano mzuri wa kuigwa katika kuchangia maendeleo ya jamii na uhifadhi endelevu, huku wakihoji ukimya wa kampuni nyingine za kitalii zaidi ya 160 zilizopo wilayani Serengeti.

 

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages