Tembo |
JITIHADA zinazofanywa na Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika kudhibiti ujamgili zimesababisha ongezeko la tembo katika maeneo ya uhifadhi nchini.
Kuongezeka kwa wanyamapori hao kumesababisha baadhi yao kuingia na kuharibu mazao ya chakula kwenye mashamba ya wananchi katika vijiji vilivyo jirani na maeneo ya uhifadhi.
Kwa upande mwingine, uchunguzi uliofanywa na Mara Online News umebaini kuwa idadi ya wananchi imeongezeka kiasi cha kuhitaji ardhi ya ziada kwa ajili ya shughuli za kilimo, malisho ya mifugo na makazi.
Aidha, viwango vya fidia zinazotolewa na Serikali kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakiwemo tembo vinalalamikiwa na wananchi kuwa ni vidogo.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi za wanyamapori wilayani Serengeti, Mara wamemwomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Damas Ndumbaro kutafuta suluhisho la kudumu la tembo wanaovamia na kuharibu mazao yao ya chakula na wakati mwingine kujeruhi na kuua watu vijijini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Damas
Ndumbaro.
“Tunamwomba Waziri wa Maliasili na Utalii aone uwezekano wa kuweka uzio wa nyaya za shoti ya umeme ili kutuokoa na tatizo la tembo,” Diwani wa Kata ya Nagusi, Andrew Mapinduzi wameiambia Mara Online News wilayani Serengeti, hivi karibuni.
Diwani Mapinduzi na wananchi wengine pia wametaka viwango vya malipo yanayotolewa kwa wananchi kama vifuta jasho na machozi kutokana na uharibifu wa mazao, watu kujeruhiwa na kuuawa na wanyamapori viboreshwe.
“Viwango vya kifuta jasho na kifuta machozi vinavyotolewa ni vya chini na haviridhishi, tunaomba hili nalo Serikali iliangalie,” amesema Mapinduzi.
Diwani huyo amesema vijiji vya kata yake vikiwemo Iharara na Singisi vimekuwa vikivamiwa na tembo wanaohatarisha maisha ya wananchi na kuharibu mazao ya chakula mashambani.
“Mbali na uharibifu wa mazao ya chakula yakiwemo mahindi, kuna watu wameuawa katika kata yangu,” amesema Mapinduzi.
Diwani wa Kata ya Nagusi, Andrew
Mapinduzi akizungumza na Mara Online News wilayani Serengeti, hivi karibuni.
Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, John Lendayane amekiri kuwepo kwa madai ya vifuta jasho na machozi kutoka wananchi walioathiriwa na wanyamapori kwa namna mbalimbali.
“Kuna wananchi wanadai lakini kwa sasa matukio ya tembo kuharibu mashamba na simba kuua na kula mifugo yamepungua kwa sasa na sio kama mwaka jana na mwaka juzi ambapo tatizo lilikuwa kubwa,” amesema Landyaone.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, hadi sasa kifuta jasho kwa mtu aliyeuawa na tembo ni Shilingi milioni moja na aliyepata jereha la kudumu ni Shilingi laki tano.
“Kwa upande wa mazao, ekari moja ya mazao yaliyoharibiwa hulipwa Shilingi 25,000 hadi Shilingi 100,000,” kimedokeza chanzo chetu cha habari.
Mbali na Serengeti, wilaya nyingine za mkoa wa Mara zenye vijiji ambavyo
vimekuwa vikiripoti matukio ya tembo kuvamia na kuharibu mazao ya chakula ni
Bunda na Tarime.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment