NEWS

Sunday 25 April 2021

Tanzania yazindua mpango wa ugawanaji maji bonde la mto Mara

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya LVBWB, Dkt Bonaventure Baya (kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt Renatus Shinhu (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dkt George Lugomela (wa pili kulia) na wawakilishi wa makatibu tawala wa mikoa ya Mara na Mwanza wakifurahia uzinduzi wa mpango wa ugawanaji maji katika bonde la mto Mara.

KWA mara kwanza Tanzania imezindua mpango wa ugawanaji maji katika bonde la mto Mara ikiwa ni hatua itakayosadia kulinda viumbe hai ndani ya mto huo na kuendeleza sekta muhimu za kiuchumi kama vile utalii, madini na kilimo.

 

Mpango huo pia utasadia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji kwa kukomesha migogoro kuhusu matumizi ya maji na kukabiliana na tishio la kimazingira linalotokana na ongezeko la idadi ya watu na shughuli za binadamu katika bonde hilo.

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amezindua mpango huo jijini Mwanza, jana Aprili 24, 2021 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga. Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Ziwa Letu wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza katika uzinduzi huo

Katika hotuba yake, Mhandisi Kemikimba amewapongeza wadau wote waliofanikisha uandaaji wa mpango huo akisema utasadia kusimamia matumizi endelevu ya maji na yenye tija katika bonde la mto Mara.

 

“Mto huu ni muhimu sana kwa ikolojia katika bonde la Mto Mara na huchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii pamoja na uhifadhi wa uoto wa asili,” amesema Naibu Katibu Mkuu huyo na kuagiza utekelezaji wa mpango huo uanze haraka na uwe na mrejesho chanya. “Tupate detailed action plan (utekelezaji wa kina wa mpango kazi),” amesisitiza.

 

Mto Mara unatajwa kuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi endelevu wa ikolojia ya Serengeti ambapo nyumbu wa Serengeti ambao ni mojawapo ya vivutio vikuu vya utalii hawawezi kuvuka bila uwepo wa mto huo.

Nyumbu wakivuka mto Mara
 

Eneo la bonde la mto Mara lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325 huku mto wenyewe ukiwa na urefu wa kilomita 400.

 

Mto huo ambao ni shirikishi kwa mataifa ya Tanzania na Kenya, unaanzia kwenye milima ya Mau na kupita katika Hifadhi ya Maasai Mara upande wa Kenya, kisha kupita Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Tanzania) na kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

 

Sehemu ya mto Mara kutokea Kenya

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyohudhuriwa pia na makatibu tawala wa mikoa ya Mwanza na Mara, miongoni mwa wadau wengine muhimu, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dkt George Lugomela amesema Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imeweka historia kwa kuwa ya kwanza kuandaa na kuzundua mpango huo ambao sasa unaweza kuwa dira katika maeneo mengine nchini.

 

Dkt Lugomela amesema kanuni zote zinazohusu rasilimaji zimezingatiwa katika kuandaa mpango huo ambao umeandaliwa na LVBWB kwa kushirikiana na wadau wake ambao ni Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) na SWP (Sustainable Water Partinership).

 

“Ni matumaini yetu kuwa wadau wataendelea kusadia utekekezaji wa mpango huu ili uwe endelevu,” Dkt Lugomela amesema na kuongeza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa Sera ya Maji ya Mwaka 2002 na Sheria ya Maji Na. 11 ya Mwaka 2009.

Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dkt George Lugomela akizungumza katika uzinduzi huo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya LVBWB, Dkt Bonaventure Baya amesema mpango huo utasadia kutatua changamoto za kimazingira zinazotishia uhai wa mto huo zikiwemo kilimo, ufugaji na uchenjuaji wa madini.

Sehemu ya bonde la mto Mara inayotumika kwa shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini
 

Dkt Baya amesema Bodi hiyo imeandaa mpango huo ili pamoja na mambo mengine, kukabiliana na changamoto hizo za kimazingira na nyingine zinazotokana na matumizi ya maji, lakini pia ongezeko la idadi ya watu kutoka 340,500 mwaka 2012 hadi 460,000 mwaka huu.

 

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo amesema kwa kuwa mto huo ni shirikishi unahitaji pia mpango wa pamoja kutoka mataifa ya Tanzania na Kenya katika kukabiliana na changamoto zilizopo.

 

Wadau husika wa mpango hupo ni pamoja na Wizara ya Maji, LVBWB, Mtaalamu Mshauri, viongozi wa Serikali ngazi za wilaya na mkoa, taasisi za elimu ya juu, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), SWP, WWF na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Tuna kila sababu ya kufurahia uzinduzi huu wa mpango wetu wa usimamizi wa rasilimali za maji mto Mara. Ndivyo wanavyelekea kusema viongozi hawa.

Dkt Baya amesema mbali na faida za kiuchumi, mpango huo utasadia kuboresha afya za wananchi na usafi wa mazingira katika bonde hilo.

 

“Faida nyingine za mpango huo ni kupunguza umaskini na kuendeleza riziki kwa wananchi wote kwa kutumia maji, lakini pia kutatua migogoro ya watumia maji na kudhibiti matumizi ya rasilimali za maji ndani ya bonde la mto Mara,” ameongeza Dkt Baya.

 

Aidha, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya LVBWB amesema mpango huo utatumika kuoanisha na kuunganisha nchi za Tanzania na Kenya ili kuwa na mpango mmoja shirikishi katika siku za usoni.

 

Viongozi wa jumuiya za watumia maji katika bonde la mto Mara wameelezea kufurahishwa na uzinduzi wa mpango huo.

 

“Hii ni habari njema sana kwetu ambayo tumekuwa tukiisubiri kwa miaka mingi. Mpango huu utatusadia kutatua migogoro ya watumia maji katika maeneo yetu,” amesema Lameck Nyasagati, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tobora yenye vijiji 24 wilayani Serengeti.

 

Nyasagati ameomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka dhidi ya uendeshaji wa shughuli za kilimo na ufugaji kwenye maeneo ya hifadhi za vyanzo vya maji akisema tatizo hilo linaendelea kuwa tishio la kimazingira katika vijiji hivyo.

Mifugo ni miongoni mwa shughuli za binadamu zinazoendelea kuongezeka katika bonde la mto Mara

“Shida iliyopo sasa hivi ni kilimo na ufugaji na inachangiwa na viongozi wa kisiasa wakati mweingine kwa kutoa matamko kwa wananchi kwa faida ya kupata kura,” amesema Nyasagati ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya LVBWB.

 

(Imeandikwa na Mugini Jacob, Mwanza)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages