NEWS

Monday 10 May 2021

Matunda ya ziara ya Rais Samia nchini Kenya yaanza kuonekana mpaka wa Sirari



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia Bunge la Kenya alipofanya ziara ya siku mbili nchini humo, wiki iliyopita.

SIKU chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kufanya ziara ya kikazi nchini Kenya, wafanyabiashara wa maeneo ya mpaka wa Sirari katika wilaya ya Tarime mkoani Mara wamesema biashara imeanza kuchangamka huku wakitabiri neema tele katika siku za mbeleni.

“Biashara nyingi hapa zilikuwa zimesimama lakini baada ya Mheshimiwa Rais Samia kuzuru Kenya na kutoa tamko, sasa mambo yameanza kubadilika na Wakenya wameanza kumiminika kwetu. Kabla ya hapo ilikuwa ni shida,” mmoja wa wafanyabiashara katika mji wa Sirari, Masafa Rhimo ameiambia Mara Online News, juzi.

Masafa amesema katika siku za nyuma Wakenya ambao ni wateja wa huduma na bidhaa mbalimbali zinazopatikan katika mji huo walikuwa wakipata adha ya kukamatwa mara kwa mara na maafisa wa uhamiaji.

“Sasa biashara itakua. Mfano wenye hoteli kama mimi tutafanya biashara na hata wafanyabiasha wa mchele watafanya biashara,” ameongeza Masafa.


Rais Samia akisaini kwenye kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili nchini Kenye kwa ziara ya siku mbili.

Mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mokare amesema ziara ya Rais Samia nchini Kenya itakuwa na faida nyingi katika kuimarisha uhusiano na biashara baina ya Wakenya na Watanzania.

“Mapokezi ya ziara ya Mama Samia nchini Kenya kwa kweli ni mazuri sana kwetu na jambo kubwa linalotatakiwa ni maelewano,” amesema Mokare amabaye ni muuzaji wa nafaka katika mji wa Sirari.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Sirari, Amos Sagara amesema ziara hiyo ya Rais Samia itafungua fursa nyingi za kibiashara katika mpaka huo, lakini akashauri Serikali kujenga masoko ya bidhaa mbalimbali, hususan mazao ya nafaka katika maeneo ya mipakani ili Wakenya wavuke kuja kuzinuua.

“Mwingiliano umeanza kuwa mkubwa, ni wakati sasa wa kujenga masoko ya mazao ya nafaka hapa mpakani ili na wenzetu waje kununua bidhaa kwetu,” amesema Sagara.


Rais Samia (kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya wakiwa katika mazungumzo Ikulu jijini Nairobi.

Diwani huyo ametoa wito kwa Serikali kufufua ujenzi wa soko ambao amesema umetelekezwa katika kijiji cha Remagwe ili liwe moja ya masoko ya kimkakati katika mpaka huo wa Sirari.

“Kuna soko hapa lilijengwa na Serikali lakini ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu, ni vizuri kumalizia ujenzi wake,” amesema.

Katika ziara hiyo, Rais Samia na Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya wameagiza kuondolewa kwa vikwazo vya biashara kwa ustawi wa mataifa hayo mawili.

(Habari: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages