NEWS

Thursday 20 May 2021

CDF yatambulisha mradi wa kutokomeza ndoa za utotoniMkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (wa tatu kushoto waliokaa), Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Koshuma Mtengeti (wa tatu kulia waliokaa) na baadhi ya washiriki wa mkutano wa kutambulisha mradi wa kutokomeza ndoa za utotoni, leo.

JUKWAA la Utu wa Mtoto (CDF) limefanya utambulisho wa mradi wa kuharakisha juhudi za pamoja kutokomeza vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni katika jamii.

Akizungumza katika mkutano wa utambulisho wa mradi huo mjini Tarime leo Mei 20, 2021, Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Koshuma Mtengeti amesema mradi huo utatekelezwa Tanzania na Kenya, hususan katika wilaya za mpakani.


Mtengeti akizungumza katika mkutano huo.

Mtengeti amesema mradi huo umeelekezwa katika maeneo hayo kwa kuwa watu wanaohusika katika ukeketaji na ndoa za utotoni wamekuwa wakikimbilia upande wa pili na hivyo kukwamisha jitihada za kukabiliana na vitendo hivyo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

“Tumeona tuungane, tushirikiane katika kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni kwa kutoa taarifa za kufichua wahusika wachukuliwe hatua za kisheria ili kuwapa watoto wa kike nafasi ya kusoma na kufikia ndoto zao,” amesema Mtengeti.


Sehemu ya washiriki wa mkutano huo.

Mtengeti amebainisha kuwa wadau wakubwa katika utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na viongozi wa Serikali wakiwemo wakuu wilaya na jeshi la polisi, viongozi wa dini, wazee na vijana.


Sehemu nyingine ya washiriki wa mkutano huo katika picha ya pamoja na Mhandisi Msafiri na Mtengeti.

Meneja Utekelezaji wa Miradi ya CDF, Evans Rwamuhuru ametaja malengo ya mradi huo kuwa ni kupunguza kama si kutokomeza ndoa za utotoni na mila zenye madhara kwa vijana, hasa watoto wa kike na jamii kwa ujumla.


Rwamuhuru akiwasilisha mada katika mkutano huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri ameushauri uongozi wa CDF pamoja na mambo mengine, kuangalia uwezekano wa kuanzisha tuzo maalum kwa waandishi bora wa habari za jinsia zinazoelimisha jamii kuachana na vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni.

“Mfano tuna gazeti letu hapa la Sauti ya Mara, tumieni waandishi wake wanaweza kutusaidia kufuatilia na kuandika habari hizi hadi vijijini,” ameongeza Mhandisi Msafiri.


Mhandisi Msafiri akizungumza katika mkutano huo.

Aidha, Mhandisi Msafiri ameushauri uongozi wa Jukwaa hilo kuwatumia watoto wa kike ambao hawakukeketwa waliofanikiwa kwa namna mbalimbali katika mpango wa kueneza elimu juu ya madhara ya mila hiyo katika jamii.

Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa wilaya amelitaka jeshi la polisi kuongeza juhudi za kuwasaka wanaoendekeza vitendo hivyo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Mtengeti, mradi huo wa kuharakisha juhudi za pamoja kutokomeza ndoa za utotoni, unafadhiliwa na Shirika la Girls Not Brides (Wasichana Siyo Wanawali) la nchini Uingereza.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages