Mifugo ikichunga ndani ya Bonde la mto Mara. |
UFUGAJI ni sehemu ya maisha ya wakazi wa mkoa wa Mara, ambapo kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Mkoa wa Mara unakadiriwa kuwa na jumla ya ng’ombe 1,651,355, mbuzi 757,428, kondoo 402,492 na kuku 1,612,672.
Idadi kubwa ya mifugo hiyo ambayo inapatikana maeneo ya vijijini.
Inakadiriwa kuwa mkoa huo una uniti za mifugo 676,160 ambazo zinahitaji eneo la malisho lenye ukubwa wa hekta 1,081,857.
Hata hivyo, taarifa zilizopo zinaonesha kuwa wafugaji wa mkoa huo ambao wengi wao wanafuga kienyeji wanakabiliwa na changamoto ya maeneo ya malisho.
Kwa mujibu wa tovuti ya mkoa wa Mara, eneo la malisho ya mifugo lililopo ni hekta 750,000, hivyo kuna upungufu wa hekta 405,697 kwa ajili ya malisho.
Moja ya maeneo ya malisho ya mifugo katika mkoa huo ni bonde la mto Mara na ufugaji ni moja ya shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Eneo la bonde la mto Mara lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325 huku mto wenyewe ukiwa na urefu wa kilomita 400.
Sehemu ya maeneo ya makazi na malisho ya mifugo katika bonde la mto Mara.
Mto huo ambao ni shirikishi kwa mataifa ya Tanzania na Kenya huanzia milima ya Mau na kupita katika Hifadhi ya Maasai Mara upande wa Kenya, kisha kupita Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Tanzania) na kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
Ufugaji unatajwa kama moja ya shughuli muhimu za kiuchumi inayotakiwa kuwa endelevu katika vijiji vilivyo jirani na mto Mara.
Hivi karibuni, Serikali ya Tanzania ilizundua mpango wa ugawanaji maji katika bonde la mto Mara (WAP) ikiwa ni hatua itakayosadia kulinda viumbe hai ndani ya mto huo na kuendeleza sekta muhimu za kiuchumi kama vile ufugaji, kilimo, utalii na madini.
Hata hivyo, mbali na umuhimu wa mto Mara, shughuli hizo za kiuchumi, hususan za ufugaji na kilimo zinachangia changamoto za kimazingira zinazotishia uhai wa mto huo.
Kwa Mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB, Dkt Bonaventure Baya, mpango wa ugawanaji maji utasadia kutatua changamoto za kimazingira zinazotishia uhai wa mto huo ikiwemo ufugaji.
Dkt Baya ansema Bodi hiyo imeandaa mpango huo ili pamoja na mambo mengine, kukabiliana na changamoto hizo za kimazingira na nyingine zinazotokana na matumizi ya maji, lakini pia ongezeko la idadi ya watu kutoka 340,500 mwaka 2012 hadi 460,000 mwaka huu.
Anaongeza kuwa mbali na faida za kiuchumi, mpango huo utasadia kuboresha afya za wananchi na usafi wa mazingira katika bonde hilo.
“Faida nyingine za mpango huo ni kupunguza umaskini na kuendeleza riziki kwa wananchi wote kwa kutumia maji, lakini pia kutatua migogoro ya watumia maji na kudhibiti matumizi ya rasilimali za maji ndani ya bonde la mto Mara,” anaongeza Dkt Baya.
Nyasagati ambaye ni kiongozi wa Jumuiya za Watumia Maji ya Tobora wilayani Serengeti, anaomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka dhidi ya uendeshaji wa shughuli za ufugaji kwenye maeneo ya hifadhi za vyanzo vya maji kwani tatizo hilo linaendelea kuwa tishio la kimazingira.
“Shida iliyopo sasa hivi ni kilimo na ufugaji na inachangiwa na viongozi wa kisiasa wakati mwingine kwa kutoa matamko kwa wananchi kwa faida ya kupata kura,” anasema Nyasagati
Kuna taarifa kuwa sehemu ya maji yanayotumiwa na mifugo hurudi katika mazingira mazingira kwa njia ya kinyesi na maji machafu.
Kinyesi cha mifugo kina idadi kubwa ya virutubisho (nitrojeni, fosforasi, potasiamu), mabaki ya dawa, metali nzito na vimelea vya magonjwa.
Ikiwa hivi vitaingia ndani ya maji au kujilimbikiza kwenye mchanga inaweza kusababisha vitisho vikuu kwenye mazingira.
Ufugaji wa mifugo bila kufuata njia za kitaalamu na uhifadhi wa mazingira sio tu unachangia matumizi na uchafuzi wa rasilimali za maji safi, bali pia unaathiri moja kwa moja kina cha maji cha mto Mara.
Ili tuweze kuhifadhi bonde la Mto Mara, lazima tubadili mfumo wa ufugaji tuweze kufuga kisasa, ingawa pia wakulima wengi hukutana na changamoto zinazowakwamisha kufuga kisasa.
Baadhi ya changamoto hizo ni upungufu wa mifugo chotara ambao umechangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji duni na usio na tija.
Hali hii imechochewa kwa kiwango kikubwa na mifumo ya uzalishaji mifugo inayotumiwa na wafugaji. Hata hivyo, mifugo ya asili ina uwezo wa kustahimili mazingira magumu.
Ukosefu wa elimu na ujuzi wa kutosha kwa wafugaji huathiri maendeleo ya mifugo nchini.
Elimu na ujuzi ni muhimu na husaidia katika kupokea teknolojia sahihi zinazobuniwa na kusambazwa kwa wafugaji.
Uchache wa taasisi za kutoa mikopo kwa wajasiriamali wakubwa, wa kati na wadogo wa mifugo na uwekezaji mdogo vinakwaza upanuzi na uzalishaji wa mifugo kibiashara.
Ikiwa changamoto zinazowakabili wakulima zitatatuliwa itawawezesha kufuga kisasa zaidi na kusaidia uhifadhi wa bonde la mto Mara kwa maslahi mapana ya jamii, lakini pia wakulima wataweza kunufaika kwa kuongeza uzalishaji wa mifugo, ubora wa mifugo na kuchangia maendeleo ya wafugaji.
(Imeandikwa na Emmanuel Daniel wa Mara Online News)
No comments:
Post a Comment