NEWS

Tuesday 11 May 2021

TANAPA yatangaza mpango wa mabalozi wa hifadhi kwa jamiiViongozi wa vijiji na kata zilizo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa wilaya ya Tarime mkoani Mara wakishiriki wa semina ya mpango wa TANAPA wa majaribio unaolenga kuwajengea wananchi dhana ya umiliki wa Hifadhi za Taifa.

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeanza kutambulisha mpango wake wa majaribio unaolenga kuwajengea wananchi dhana ya umiliki ili waweze kushiriki kikamilifu katika ulinzi na utunzaji wa maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.

Kwa kuanzia, mpango huo utatekelezwa katika baadhi ya vijiji vilivyo jirani na Hifadhi za Taifa za Serengeti na Ruaha.

Kwa upande wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mpango huo utatekelezwa katika vijiji 16 vilivyopo katika wilaya za Tarime, Bunda, Bariadi na Serengeti.


Washiriki wakifuatilia mada katika semina hiyo.

Katika wilaya ya Tarime, mpango huo umeanza kutambulishwa leo Mei 11, 2021 kwa njia ya semina kwa viongozi wa vijiji vya Karakatonga, Kegonga, Masurura, Nyabilongo na kata za Kwihancha, Nyanungu na Gorong’a.

“Mpango huu ni wa kuwajengea wananchi uelewa wa masuala ya uhifadhi ili watambue kuwa wana wajibu wa kulinda na kutunza hifadhi za taifa,” Mkuu wa Idara ya Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard amesema katika semina hiyo iliyofanyika katani Nyamwaga.


Mhifadhi Hobokela (aliyesimama) akizungumza katika semina hiyo.

Mhifadhi Hobokela amesema baada ya semina hiyo, wahifadhi watapita katika kila kijiji husika kuteua mwakilishi wa Hifadhi kwa jamii - mwenye elimu ya sekondari na kuendelea.

Katika semina hiyo, Hobokela ameshirikiana na wahifadhi wenzake, Seph Choma, Zabron Mtweve, Julius Katambi na Njonga William kuwasilisha mada za wasifu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mpango wa ujirani mwema, sheria za hifadhi za taifa na mpango wa kufanya kazi na jamii.


Mhifadhi Choma akiwasilisha mada ya wasifu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Victoria Mapesa amesema semina hiyo itajenga na kuimarisha uhusiano na ujirani mwema kati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na wakazi wa vijiji jirani.

Awali akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri ameipongeza TANAPA akisema mpango huo utasaidia kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori.


Mhandisi Msafiri (aliyesimama) akifungua semina hiyo.

Mhandisi Msafiri ametumia nafasi hiyo pia kuwashauri wana-Tarime wanaoishi katika vijiji vilivyo jirani na hifadhi hiyo kuangalia uwezekano wa kutenga eneo kwa ajili ya kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Management Area - WMA) itakayowaingizia fedha za kigeni kutokana na uwekezaji wa hoteli na kambi za kitalii.

(Habari na picha: Mara Online News)

1 comment:

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages