WAKAZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) wametakiwa kupuuza uvumi unaosambazwa kuwa serikali imeanza kutoa chanjo wa kuzuia virusi vya ugonjwa wa korona kwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani hapa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Tarime (Vijijini), Dkt Joseph Ngowi akimpa dawa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Maika, Janet Gikaro.
Akizindua mpango wa umezaji dawa za minyoo na kichocho kwa watoto chini ya miaka 14, uliofanyika Shule ya Msingi Nyamwaga, Kaimu Mkurugezi ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo (DMO), Joseph Ngowi amesema kuwa zoezi hilo ni la kawaida hufanyika kila Mwaka.
“Leo hatutoi chanjo ya korona hapa kama wanavyo potosha mitaani tunagawa dawa za ugonjwa wa minyoo na kichocho katika shule zote hivyo puuzeni uvumi huo na tukiwabaini wanatangaza habari hizo tutawashugulikia,” alionya Dkt Ngowi.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Mratibu wa magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele, Dkt Deogratius Nyanza amesema wanatarajia kugawa dozi kwa watoto 102,606 wenye umri chini ya miaka 14 katika shule 139 za Tarime Vijijini.
Mwanafunzi wa darasa la saba, Philemon Tereli akimeza dawa mbele ya Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt Joseph Ngowi.
“Dawa zitakazotolewa leo ni aina mbili ambazo ni Praziquantel kwa ajili ya kutibu kichocho, tumbo na kibofu na Albendazole ni kwa ajili ya kutibu minyoo ya tumbo aina zote kwani ni salama baada ya kuthibitishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA),” alisema Dkt Nyanza.
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) ni miongoni mwa halmashauri tisa za mkoa wa Mara ambazo zimefanya shughuli hiyo Mei 26, mwaka huu kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa usimamizi wa walimu wao baada ya kupewa chakula shuleni.
(Habari na picha: Mobini Sarya)
No comments:
Post a Comment