NEWS

Sunday, 21 December 2025

RC Mara atoa siku 30 kwa Jeshi la Polisi kuachia jengo la Ushirika wa WAMACU



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 16 wa WAMACU Ltd huo mjini Tarime, Ijumaa iliyopita.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
----------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amemwagiza Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, kusimamia urejeshaji wa jengo la Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) lililokodishwa kwa Jeshi la Polisi.

Kwa miaka kadhaa sasa, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime-Rorya limekuwa likitumia jengo la WAMACU lililopo mjini Tarime kwa kukodi wakati likisubiri ujenzi wa jengo lake.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya WAMACU iliyowasilishwa kwa RC Mtambi wakati wa Mkutano Mkuu wa 16 wa ushirika huo uliofanyika mjini Tarime Ijumaa iliyopita, jeshi hilo ni kama limegoma kuachia jengo hilo.


Wajumbe mkutanoni

Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, Momanyi Range, alilalamika mbele ya RC Mtambi kwamba ushirika huo una watumishi wengi ambao wanahitaji ofisi za kuendeshea shughuli zao.

“Ndugu mgeni rasmi, changamoto kubwa tuliyo nayo ni jengo la union [ushirika huo] ambalo lilipangishwa kwa Kanda Maalum ambao wamekataa kutoka na wamelibadilishia matumizi,” alisema Range na kuendelea:

“Nimekuwa nikipata malalamiko kutoka kwa wanachama wa union wakidai uongozi umeuza majengo - mali yao inatumika kwa matumizi ambayo si ya kwao wakati wao ni wahitaji.

“Sasa hivi tuna watumishi wengi, tunahitaji ofisi, magari uliyozindua yanahitaji kupimwa uzito, kwenye jengo hilo kuna mizani ya kupima uzito mkubwa. Tunaomba utusaidie tukabidhiwe jengo letu kwa ajili kulitumia kwa manufaa ya ushirika wetu.”

Kutokana na malalamiko hayo, RC Mtambi alimwagiza DC Gowele kusimamia ili kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi ndani ya siku 30.

“Niwapongeze WAMACU kwa kuwapa wenzetu wa Kanda Maalum eneo la kufanyia kazi wakati wanajenga la kwao. DC nakupa mwezi mmoja jamaa zetu wawe wameachia jengo lile ili mwakani WAMACU waweze kuendelea kutanua shughuli zao, ukishindwa niambie nije nikusaidie,” aliagiza.

Mkutano huo wa WAMACU ulilenga kujadili na kutathmimi mambo yaliyotelekezwa kwa mwaka 2025/2026 na kupitisha mpango wa shughuli zake kwa mwaka 2026/2027.

Mbali na kuhutubia mkutano huo, RC Mtambi alizindua vyombo vya usafiri na usafirishaji ikiwa ni pamoja na kenta mbili, Scania mbili, bajaji za mizigo mbili na pikipiki saba vilivyonunuliwa na WAMACU kwa shilingi milioni 596.


RC Mtambi akizindua vyombo hivyo vya usafirishaji


Sehemu ya vyombo vipya vya usafirishaji vilivyonunuliwa na WAMACU Ltd

Mkuu wa Mkoa pia alikagua na kuzindua kitalu cha miche bora ya kahawa zaidi ya 800,000 kilichopo eneo la kiwanda cha kuchakata kahawa kinachomilikiwa na ushirika huo mjini Tarime.

Katika hotuba yake, RC Mtambi alieleza kufurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na WAMACU kuinua kilimo, na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuziunga mkono ili kuwasaidia wakulima kufikia malengo yao ya kiuchumi na kijamii.

"Ushirika wenu huu umenifurahisha, mko kwenye maeneo yote, usafirishaji - mmeanzia pikipiki, bajaji, kenta, mna maghala, kituo cha mafuta, gereji na kuajiri maafisa kilimo mbalimbali.

"WAMACU ni ushirika unaojipambanua. Kama Serikali ya Mkoa na Serikali Kuu, ninawaahidi ushirikiano wowote mtakaohitaji kutoka serikalini tutakupatieni, wataalamu mtakaotaka mtapata,” alisema kiongozi huyo wa mkoa.


RC Mtambi alitumia fursa hiyo pia kutoa maelekezo mbalimbali kwa WAMACU, ikiwemo kukamilisha usajili wa wanachama wapya, kusimamia Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) na ajira za watendaji wenye ujuzi na weledi ili kujiimarisha katika mifumo ya TEHAMA.

Vilevile, aliuelekeza ushirika huo kupanua wigo hadi kwenye mazao mengine ya kimkakati kama vile chai na choroka, badala ya kujikita zaidi kwenye kahawa na tumbaku tu.

“WAMACU mmekuwa mkijikita kwenye kahawa, lakini kuna mazao mengine ya kimkakati. Tarime kuna kilimo cha chai lakini siwaoni kwenye chai. Wakulima wa mkoani Mara pia wameanza kufanya vizuri kwenye zao la choroko - kule pia hampo, sasa hivi mmeanza kuingia kidogo kwenye tumbaku.

“Sasa nitoe rai kwenu, hebu mjitanue kwenye mazao mengine haya ya kimkakati… WAMACU si kahawa tu – tuko kwenye mazao yote, niwatie shime nendeni muwafikie wakulima wote wa mkoa wa Mara,” alisema RC Mtrambi.

Kwa upande mwingine, aliwakumbusha wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kusimamia uratibu na uzalishaji wa mazao yenye tija na kudhibiti upotevu wa mazao baada ya uvunaji.

Aliwalekeza kutekeleza pia kusimamia ubora wa mazao yanayoingia sokoni ili yauzike kwa bei nzuri kwa manufaa ya wakulima.

Awali, Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Marwa Gisiboye, pamoja na mambo mengine, alimweleza mgeni rasmi namna ushirika huo utakavyonufaika na vyombo vipya vya usafirishaji vilivyonunuliwa.

"Magari haya yatachochea biashara na mapato kuongezeka na yatarahisisha ufikaji wa kahawa kiwandani kwa haraka, hivyo kuepusha kahawa kunyeshewa na kuharibika. Pia yamepunguza changamoto ya kukodi magari.

"Kwa msimu mzima mmoja tunaenda hadi tripu 850. Mfano, sasa tumeenda tripu 887. Kukodi magari ilikuwa changamoto kubwa,” alieleza GM Gisiboye katika sehemu ya taarifa yake.


GM Gisiboye akizungumza katika mkutano huo

WAMACU Ltd ni miongoni mwa vyama vikuu vya ushirika vilivyopewa kusimamia usambazaji wa mbolea za ruzuku ya serikali kwa wakulima kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), TFC na OCP.

Ushirika huo una leseni ya kuuza kahawa nje ya nchi kama vile Uingereza na Marekani, baada ya kuikusanya kutoka kwa wakulima kupitia AMCOS na kuiongezea thamani.

Aidha, kwa sasa ushirika huo una leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo, ikiwemo mbolea kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

Wadau wakubwa wanaoshirikiana na WAMACU kutekeleza miradi yake ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), wataalamu wa kilimo kutoka halmashauri za wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

TADB inatajwa kuchochea maendeleo ya zao la kahawa mkoani Mara kupitia WAMACU, hasa katika ununuzi wa mitambo ya kubangua kahawa kavu na mbivu, dhamana na mkopo wa miche kwa awamu ya kwanza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages