NEWS

Monday 17 May 2021

Mto ‘waua’ kilimo cha mpunga RoryaSehemu ya eneo lenye ukubwa wa ekari 350 kijijini Chereche, Rorya lililofurika maji na kuzuia kilimo cha mpunga tangu Aprili 2018.

KITENDO cha mto Mori kuacha mkondo wake kimezua balaa ikiwemo ‘kuua’ kilimo cha mpunga kwa kujaza maji katika eneo lenye ukubwa wa ekari 350 ambalo mamia ya wananchi wamekuwa wakilitumika kulima zao hilo katika kijiji cha Chereche wilayani Rorya, Mara.

Wenyeji wanasema mto huo ulianza kuelekeza maji nje ya mkondo wake wa asili tangu Aprili 2018 na kubomoa ukuta wa bwawa la maji la mradi wa Ushirika wa Wakulima wa Mpunga Chereche Rorya (UWACHERO).

“Maji ya mto huo yalivunja tuta [ukuta] la skimu UWACHERO, maji yakafurika na kutuzuia kuendesha kilimo cha mpunga kwenye bonde la Chereche lenye ukubwa wa ekari 350,” Mwenyekiti wa UWACHERO, Thobias Omoro ameiambia Mara Online News kijijini hapo, hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Omoro, wastani wa uzalishaji wa mpunga katika eneo hilo ulikuwa tani 5,000 kwa kila msimu na kwamba wananchi zaidi ya 300 waliokuwa wanategemea kilimo hicho kwa ajili ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha na familia zao wameathirika kiuchumi.

“Baadhi ya vijana waliokuwa wanalima mpunga katika bonde hili wameanza kujihusisha na vitendo vya udokozi. Hivi karibuni watatu kutoka vijiji vya Mori na Chereche walikamatwa na kufikishwa polisi kwa tuhuma ya kuiba ng’ombe wa kisasa,” anasema kiongozi huyo wa UWACHERO.

Mchepuko mto Mori ulianzia hapa

Madhara mengine
Mbali na kuzuia kilimo cha mpunga, mchepuko wa mto Mori umewalazimu baadhi ya wanakijiji waliokuwa wanaishi jirani na bonde la Chereche kuhama baada ya makazi yao kuvamiwa na mafuriko kutokana mchepuko wa mto huo.

“Wananchi waliovamiwa na mafuriko ya mto Mori kwenye makazi yao wamekimbilia maeneo ya mwinuko. Hata kwenye kitongoji cha Nyarugusu maji yamevamia na kutwama kwenye makazi ya watu,

“Baadhi ya maeneo ya kulima mahindi na mtama katika kitongoji cha Nyarugusu na hata huku Chereche yamegeuka pori la matende, hata ng’ombe akiingia kuchunga anakwama kwenye tope.

“Kwa ufupi hali ikiendelea hivi makazi mengi ya watu yatavamiwa na maji na wananchi wengi tutakabiliwa na njaa kubwa zaidi,” anasema mkazi wa Chereche, Lameck Ayuke.


Mkazi wa kijiji cha Chereche, Lameck Ayuke akionesha mto Mri ulivyoacha mkondo wake na kuelekeza maji kwenye maeneo ya kilimo kijiji Chereche.


Ng'ombe wakichunga pembezoni mwa eneo lililovamiwa na maji ya mto Mori katika kijiji cha Chereche.

Aidha, mawasiliano kati ya wakazi wa Nyarugusu na Chereche yamekuwa ya shida baada ya maji ya mto Mori kubomoa ukuta wa bwawa la maji la mradi wa UWACHERO waliokuwa wanatumia kama daraja la kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Waathirika wakubwa wa hali hiyo ni wakazi wa Nyarugusu ambao wanategemea kufuata huduma muhimu za kijami zikiwemo za elimu na afya upande wa Chereche.

“Tunapata shida sana … ukuta huu ulikuwa unaunganisha kitongoji cha Nyarugusu na cha Obolo, lakini baada ya mto Mori kupoteza uelekeo na kuelekeza maji katika bwawa hili la UWACHERO, kitendo hicho kilisababisha bwawa kuzidiwa na ukingo wake kubomoka na kusababisha madhara makubwa.

“Kwanza mawasiliano kati ya kitongoji cha Obolo na cha Nyarugusu ambacho sasa kimekuwa kama kisiwa ni ya shida sana, tunavuka kwa kutumia chombo cha mbao kama mtumbwi kinachovutwa kwa kamba.

“Chombo hiki wakati maji yanapokuwa mengi watu hawawezi kuvuka, ina maana shughuli hata huduma muhimu za kila siku haziwezi kupatikana. Mfano wakazi wa Nyarugusu wanafuata mahemezi yote ya kifamilia katika kijiji cha Chereche, lakini maji yakishajaa hawawezi kuvuka.

“Mfano mama mjamzito anataka kujifungua, maji yamejaa, wanafunzi wakati fulani wanachelewa shule kwa sababu ya maji kujaa,” anasema Mwikwabe Wambura, mkazi wa kitongoji cha Obolo kijijini Chereche na kuongeza:

“Lakini zaidi, eneo hili limekuwa hatarishi sana kwa maisha ya mwanadamu, watu wawili wameshapoteza uhai hapa, kuna mwanafunzi wa darasa la sita alipoteza uhai kwa kuzama majini, pia kuna mzee alizama katika eneo hili.”

Mkazi wa kitongozi cha Nyarugusu akitumia chombo cha kuvuta na kamba kuvuka maji ya mto Mori kwenda kitongoji cha Obolo kijijini Chereche.

Wakazi wengine wa Chereche, Mapinduzi Sanya na aliyejitambulisha kwa jina moja la Lucia wanakiri kutokea kwa vifo vya watu wawili katika eneo hilo.

“Watu wawili wameshakufa hapa, mmoja akijaribu kuogelea na mwingine akijaribu kuvuka, ukiteleza tu basi, na kwenye kuogelea hapa maji yanazunguka, kwa kweli tunateseka sana,” anasema Wambura.

“Kwa hiyo,” Wambura anasema “Kulingana na adha tunazopata, tunaomba msaada wa Serikali izibe ukuta uliobomolewa ili shughuli za awali zirudi, lakini pia wananchi wa huku warudi katika ‘system’ yao ya awali. Lakini ili kurekebisha eneo hili, waanzie kule ambako mto Mori ulianzia kupoteza mwelekeo.”

Hata hivyo, Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imeanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha mto huo kuacha mkondo wake, kwa mujibu wa Afisa Uhusiano wa Bodi hiyo, Mhandisi Gerald Itimbula.

(Habari na picha: Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages