NEWS

Saturday, 14 February 2026

Serikali ifanyie kazi wazo la kujenga kituo cha utalii wa utamaduni Sirari




Na Mwandishi Wetu
----------------------------

Wazo lililotolewa hivi karibuni na vijana wa Tarime la kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kujenga kituo maalum cha utalii wa utamaduni katika mji wa Sirari, ni la msingi na lenye maono mapana ya maendeleo.

Ni wazo linalopaswa kuungwa mkono kikamilifu kwa mustakabali wa utalii wa kitamaduni wa wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara na nchi ya Tanzania kwa ujumla.

Vijana wa Tarime waliwasilisha wazo hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, katika mkutano maalum ulioandaliwa na Chifu wa Koo ya Wakenye, Christopher Mwita Gachuma, na kuhudhuriwa pia na Chifu wa Koo ya Watimbaru, Peter Zakaria.

Wazo hilo linaonesha wazi kuwa vijana wa Tarime wameamka na wanatambua thamani ya urithi wa kitamaduni kama rasilimali ya kiuchumi.

Sirari ni mji wa kimkakati uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya. Kila siku, mamia hadi maelfu ya wasafiri, wafanyabiashara na watalii hupita katika mpaka huo.

Hata hivyo, kwa muda mrefu mji wa Sirari umekuwa ni kituo cha mpito tu, badala ya kuwa lango la kutangaza utamaduni na utambulisho wa jamii za Tarime.

Kujengwa kwa kituo maalum cha utalii wa kitamaduni kutabadilisha hali hiyo na kuifanya mji wa Sirari kuwa kivutio cha kudumu, badala ya njia ya kupita pekee.

Wilaya ya Tarime ina hazina kubwa ya tamaduni, sanaa, mila na desturi nzuri - kuanzia ngoma za asili, mavazi ya kimila, vyakula vya jadi, historia za koo na mifumo ya kijamii iliyojengwa kwa mshikamano na heshima.

Kituo cha utalii wa kitamaduni kitatoa jukwaa rasmi la kuonesha urithi huo, huku kikisaidia kuuhifadhi dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaosababishwa na mabadiliko ya kijamii na utandawazi.

Zaidi ya hilo, mradi huo utakuwa na mchango mkubwa katika ajira na uchumi kwa vijana. Wasanii wa ngoma za asili, muziki, wachongaji, wabunifu wa mavazi ya asili, waongozaji wa watalii na wajasiriamali wadogo watanufaika moja kwa moja.

Badala ya vijana wengi kukimbilia mijini au kujiingiza katika shughuli zisizo na tija, watapata fursa za halali za kipato kupitia utamaduni wa eneo la wenyewe.

Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kukuza utalii wa ndani na wa kipekee unaotegemea rasilimali za maeneo husika.

Hivyo, wazo la vijana wa Tarime linaendana kikamilifu na dira hiyo. Ni wakati sasa wa kuliona kama pendekezo la kimkakati la maendeleo ya kikanda na kitaifa.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kushirikiana na mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime iangalie uwezekano wa kulifanyia kazi wazo hilo kwa vitendo.

Utafiti wa haraka wa uwezekano, ushirikishwaji wa viongozi wa kimila kama Chifu Gachuma na Chifu Zakaria, pamoja na vijana wenyewe, ni hatua muhimu za awali.

Mji wa Sirari una nafasi ya kuwa alama mpya ya utalii wa kitamaduni katika Kanda wa Ziwa na mpakani mwa Tanzania na Kenya. Kupuuza fursa hii ni kupuuza sauti ya vijana, urithi wa utamaduni na chanzo kipya cha maendeleo.

Hivyo basi, serikali izingatie wazo hilo la vijana, ichukue hatua na iufungue mji wa Sirari kuwa dirisha la utalii na utambulisho wa Tarime kimataifa.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages