NEWS

Sunday 2 May 2021

Naibu Waziri Waitara ajuta kuingizwa chaka Nyamongo

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amelaani kitendo cha kupigiwa simu na kudanganywa kuwa vijana watano wamefukiwa shimoni katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ilhali hakukuwa na tukio hilo.

 

Waitara amakemea kitendo hicho kwa nyakati tofauti jana Mei 2, 2021 kwenye mikutano ya hadhara katika vijiji vya Komarera na Nyakunguru wilayani Tarime, alikokwenda kuhimiza wananchi wanaohamishwa kupisha shughuli za mgodi huo kuhakikisha wanakuwa waaminifu na wakweli katika mpango wa tathmini na malipo ya fidia za mali zao mbalimbali.

Shughuli zikiendelea katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara
 

“Baada ya kuambiwa taarifa hizo nilimpigia simu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini wakaelekeza ikaundwa timu maalum ikikatumia gharama kubwa kwenda kuchunguza ikiwa ni pamoja na kutumia grader kutoboa mashimo kule mgodini, kumbe nilikuwa nimeingizwa chaka, vijana waliodaiwa kufukiwa kumbe walikuwa wanakula maisha, tulifuatilia walikokuwa wamejifungia tukakuta chupa za K Vant, Konyagi na mifupa ya kuku wa kienyeji imejaa.

 

“Baadaye napigiwa simu na vijana hao wanasema waambie ndugu zetu wasifanye matanga na kugawana mali zetu sisi tuko hai hatujafa… hiyo imenipa fundisho, kumbe watu walikuwa mitaani wanakula maisha, nimeingizwa chaka,” amesema Waitara.

 

Akihutubia mkutano wa kijijini Komarera ambako wananchi wanasubiri kufanyiwa tathmini ya maeneo yao, Mbunge Waitara amewataka walengwa wa mpango huo kutoa ushirikiano na kuepuka vitendo vya kughushi na udanganyifu ili haki itendeke kwa kila upande.

Wakazi wa kijiji cha Komarera wakimsikiliza Mbunge Waitara (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara kijijini hapo, jana.
 

“Nawaomba sana wakati wa tathmini kila mtu asimame kwenye eneo lake na ukishalipwa kwa bei ya soko ondoka ukafanye maendeleo yako. Ninataka haki itendeke, na hili nitalisimamia. Mimi kama mbunge sifurahii kuona watu wangu wanashtakiwa.

 

“Kama kuna mtu anapanga kudanganya kwenye zoezi hili ukikamatwa kwa kesi ya kughushi utashtakiwa kwa uhujumu uchumi, na sisi hatutakuwa na uwezo wa kukusaidia. Kwa hiyo msikubali kutumika na kuingizwa mjini, utakamatwa wewe aliyekutumia atakuruka - kesi itakuwa yako. Naomba chondechonde kila mtu asimame kwenye eneo lake.

 

“Rais Samia Suluhu Hassan anasema tuwe waadilifu, ridhika na chako cha halali hata kama ni kidogo, ukitaka vingi visivyo vya halali utapata shida. Mnisaidie niwatetee kwa kuwa wakweli na kutoa taarifa za kweli.

 

“Ikitokea mtu amekamatwa kwa kudanganya safari hii sitasema kwanza, nitafuatilia nikikuta ameonewa nitamtetea. Nikitetea waongo Serikali haitaendelea kuniamini, kwa hiyo atakayedanganya sitamtetea ila atakayeonewa nitakuwa wakili wake na kipaza sauti chake,” amesisitiza Waitara.

 

Katika mkutano wa kijijini Nyakunguru ambako wananchi wanasubiri kulipwa fidia za mali kwa miaka minane sasa tangu maeneo yao yalipofanyiwa tathmini na kuzuiwa kuyatumia kwa shughuli yoyote ile, Mbunge Waitara amewambia sasa wakae mkao wa kula kwani ana taarifa kutoka serikalini kwamba mpango wa kuwalipa utaanza kutekelezwa wiki ya kwanza ya Mei 2021.

 

Inaelezwa kwamba wanakijiji hao wamecheleweshewa malipo ya fidia zao baada ya kubainika kuwa wachache miongoni mwao walighushi umiliki wa maeneo yaliyofanyiwa tathmini.

 

(Habari na Picha: Mara Online News) 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages