NEWS

Sunday 2 May 2021

Wananchi walalamika kwa Waitara walivyosotea fidia zao mgodi wa North Mara

Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Nyakunguru wakimsikiliza Mbunge wao wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Nyamichele, leo.

WANANCHI wa kijiji cha Nyakunguru kilichopo jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara wamefunguka mazito mbele ya Mbunge wa jimbo hilo, Mwita Waitara, wakilalamika kucheleweshewa fidia za mali zao mbalimbali kwa miaka minane sasa, baada ya kufanyiwa tathmini na kutakiwa kuhama ili kupisha shughuli za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

 

Mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

 

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mbunge Waitara katika kitongoji cha Nyamichele leo Mei 2, 2021, wanakijiji hao wamemwomba kiongozi wao huyo kuingilia kati suala hilo ili waweze kupata haki yao hiyo ambayo wameisubiri kwa muda mrefu.

 

Mmoja wa wawakilishi wa wananchi hao, Samwel Peter Timasi amesema kucheleweshewa fidia hizo kumesababisha wanakijiji wengi kuishi na familia zao katika hali ya kimaskini kwa kuwa hawaruhusiwi tena kutumia maeneo yao yaliyofanyiwa tathmini kuendesha shughuli zozote zile zikiwemo za uzalishaji mali.

 

Akijibu malalamiko hayo, Mbunge Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, amesema viongozi husika serikalini wameshamwambia suala la malipo ya fidia zao litaanza kushughulikiwa kuanzia wiki inayoanza kesho Jumatatu.

Mbunge Waitara akihutubia wananchi wa kijiji cha Nyakunguru.

Waitara amesema taarifa alizonazo kutoka serikalini ni kwamba fidia za mali za wananchi hao ilikuwa zianze kulipwa mwaka jana na mapema mwaka huu lakini mpango huo ulikwazwa na janga la virusi vya corona na kifo cha Rais Dkt John Pombe Magufuli.

 

Hata hivyo, kiongozi huyo amewahakikishia wanakijiji hao kwamba ataendelea kushirikiana na viongozi wengine kufuatilia kwa karibu mchakato huo ili kuhakikisha kuwa wananchi wote waliofanyiwa tathmini halali ya mali zao wanalipwa kipindi hiki.

 

Kabla ya kwenda kijijini Nyakunguru, Waitara ameanza kuhutubia mkutano wa hadhara wa wananchi wa kijiji cha Komarera wanaoelekea kuhamishwa ili kupisha mgodi wa North Mara kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini.

Wananchi wa kijiji cha Komarera wakimpungia mikono Mbunge Waitara katika mkutano wa hadhara kijijini hapo, leo.

Mbunge Waitara ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wananchi wa vijiji hivyo kuhakikisha kila mmoja anasimama kwenye eneo lake wakati wa tathmini na malipo ya fidia na kuepuka vitendo vya kughushi na udanganyifu kwani vinaweza kuwaingiza katika matatizo ya kushtakiwa, lakini pia kukwamisha utekelezaji wa mpango huo.

 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages