NEWS

Monday 17 May 2021

Nishati mbadala ni suluhisho la uharibifu wa mazingiraMwananchi akisafirisha mkaa kutoka kijiji cha Kwisaro kupeleka kuuza mjini Musoma.

TAKWIMU za kitaalamu zinaonesha kuwa kila siku ekari zaidi ya 10,000 zinaharibiwa kwa ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya mkaa na matumizi mengine hapa nchini Tanzania.

Katika mkoa wa Mara, ekari nyingi za misitu ya asili katika bonde la mto Mara zimeharibiwa kutokana na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Mairi Magabe, Mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji katika eneo oevu la Mara Kusini, anakiri kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa misitu mingi ikitoweka kutokana na uhitaji wa nishati hizo.

“Miaka ya nyuma ulitakiwa ukatize katikati ya msitu wa miti mingi ili uweze kufikia eneo la maji ya mto [Mara], lakini sasa miti mingi imekatwa eneo hili, ukitaka unapita hadi mtoni bila kukutana na misitu ya miti,” Magabe ameiambia Mara Online News, kijijini Kwisaro, hivi karibuni.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Tatu Steven anaeleza kuwa hali ya miti katika kijiji chao kwa sasa imepungua kutokana na matumizi mbalimbali ya binadamu.

“Ni kweli eneo hili lilikuwa na miti sana lakini sasa hivi miti mingi imeshakatwa kwa sababu ndiyo tunatumia nyumbani kama kuni na matumizi mengine,” anasema.

Naye Thomas Marwa ambaye ni mfugaji kutoka kijiji cha Kwisaro anasema watu wanaoishi maeneo ya mijini, wengi wao wamechangia misitu ya miti kijijini hapo kutoweka kwani wao ndio watumiaji wakubwa wa nishati ya mkaa.

“Hapa watu wengi zaidi wamekuwa wanakata mkaa na kwenda kuuza maeneo ya mjini huko Musoma kwa sababu wakifika kule wanapata pesa nyingi zaidi,” anasema Marwa.


Wananchi wakitumia usafiri wa baiskeli kusafirisha mkaa kutoka kijiji Kwisaro kwenda kuuza mjini Musoma.

Matumizi ya nishati ya kuni hayana athari kwenye mazingira pekee, bali pia hata kwenye afya za watu, ambapo Tatu anasema kutumia kuni kwa muda mrefu kumesababisha macho yake kuwa na uoni hafifu.

“Wakati mwingine ikifika jioni nashindwa kuona vizuri hata siwezi kusoma, nimekuwa nikiumia sana na moshi wa kuni wakati wa kupika,” anasema Tatu.

Mbali na kuathari macho, Daktari wa magonjwa ya binadamu, Godfrey Samson anasema athari za moshi wa kuni zinaweza kumpata mtu hata katika mfumo wa upumuaji.

“Mtu anapovuta moshi utakanao na kuni huenda kwenye mapafu na hivyo kusababisha uzalishaji wa hewa ya oxygen kwenye mwili kuwa mdogo na anaweza kupata athari katika upumuaji, ambapo pia anaweza kupata magonjwa mengine kama majipu kwenye mapafu,” anasema Dkt Samson.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, baadhi ya mashirika yameweza kuchukua hatua za kuokoa mazingira kutokana na matumizi ya miti kama nishati.

Magabe anasema wameweza kupata mafunzo ya kutengeneza majiko ambayo hutumia nishati kidogo ya mkaa, kutoka Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF).

“Kuna wataalamu wamekuja kutusaidia jinsi ya kutengeneza majiko banifu, ambayo hutumia mkaa kidogo katika kupika, lakini bado yanatumia nishati ya mkaa,” anasema.

Kipato duni kwa wakazi wa kijiji cha Kwisaro ndio sababu kubwa ya wananchi kutumia kuni na mkaa kwani nishati mbadala imeonekana ni ghali, hali inayowalazimu watu wengi kuendelea kutumia mkaa.

Magabe anakiri kuwa ni vigumu kwa mwananchi wa kawaida kuweza kumudu kununua gesi kwa ajili ya matumizi ya matumizi ya nyumbani.

“Kutokana na umaskini na ukosefu wa pesa, watu wengi hujiingiza kwenye shughuli ya ukataji miti na kuchoma mkaa ili wakauze mijini waweze kupata pesa, ndio njia rahisi ya watu kupata pesa huku,” anafafanua.

Sababu nyingine za Watanzania wengi kutumia nishati ya mkaa ni za kiutamaduni na mazoea.

Mazoea ya kutumia nishati ya mkaa yanawaaminisha wengi kwamba nishati hiyo huivisha vizuri chakula kama vile maharage, wali na kadhalika, ikilinganishwa na nishati ya gesi, au umeme.

Wanamazingira wanapendekeza kuwa nishati za gesi, umeme na jua zinafaa kutumiwa kwa kuwa haziharibu mazingira.

Nishati nyingine inayopendekezwa ni ya bayogesi (inayotokana na uozo wa masalia mbalimbali ya vyakula na hata vinyesi vya wanyama) na mkaa unaotokana na masalia ya uchafu/takataka za nyumbani, mfano vifuu vya nazi, pumba za mbao, maganda ya korosho na magunzi ya mahindi.

Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Julius Nyerere aliwahi kusema “Elewa kuna kitu kinaitwa wizi, wizi wote ni mbaya, lakini wizi mbaya kupita wote ni kumuibia mtoto wako ambaye hajazaliwa, ni kumuibia mjukuu, unaiba mali yake. Kuharibu mazingira ni kuiba mali ya vizazi ambavyo havijazaliwa.”

(Imeandikwa na Emamanuel Daniel)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages