NEWS

Sunday, 28 December 2025

TRA Mara yawaelimisha bodaboda taratibu za kuvusha bidhaa mpaka wa Sirari



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akifungua semina ya mafunzo kwa bodaboda katika mji mdogo wa Sirari.

Na Godfrey Marwa
Tarime
----------

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imeendesha semina ya kuwaelimisha maafisa usafirishaji (bodaboda) taratibu na sheria za uingizaji na utoaji bidhaa nchini.

Semina hiyo ilifanyika hivi karibuni katika mji mdogo wa Sirari uliopo mpakani na nchi ya Kenya, kwa kuwakutanisha maafisa usafirishaj hao, viongozi wa chama na serikali, Jeshi la Polisi, wataalamu wa kilimo na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, alisema bodaboda wanapaswa kujenga ushirikiano na mamlaka husika ili kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

"Bodaboda ni kazi rasmi kama zilivyo kazi zingine, tutengeneze mazingira mazuri ya ufanyaji kazi kwa pamoja - kati ya wataalamu, wasimamizi na viongozi kwenye maeneo yenu.

"Wakati mwingine tunakamatana kwa kutokuwa waelewa, tungeweza tukanunua bidhaa maafisa wakatusaidia tukalipia tukapita vizuri [mpakani] kazi zikaendelea. Mtu anapigwa faini ya shilingi 50,000 ana familia watoto wanamtegemea, marejesho huyu mtu lazima tumsaidie.

"Tujitambue, wengine wamekopa mikopo hailipiki - hajui sheria, akikamatwa na magendo huko chombo kinataifishwa, tumeona ni vyema tukawaelimisha, tunaumia kwa kukosa maarifa,” alisema DC Gowele.

Aidha, aliwaomba maafisa usafirishaji kuwa mabalozi wazuri kwa kupeleka taarifa za uhalifu, ukiwemo wa magendo ili serikali iongeze mapato waweze kupata mikopo yenye riba nafuu.

Awali, Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Mara, Abdallah Mambi, alimweleza mgeni rasmi kwamba semina hiyo ni muhimu kwa bodaboda kwani wanatumika kusafirisha bidhaa ndogo ndogo kuingia na kutoka nchini.

Pamoja na mambo mengine, Mambi aliwaelimisha bodaboda hao madhara ya bishara ya magendo, hivyo akawataka wabadilike kwa kuhakikisha wanafuata taratibu zilizoweka na serikali, ikiwa ni pamoja na kupita kwenye njia halali.

Kwa upande wake, Katibu wa Maafisa Usafirishaji Wilaya ya Tarime, Dickson Christopher, aliishukuru TRA kwa kuwapa elimu hiyo muhimu kwa ustawi wao na Taifa kwa ujumla.

Vilevile, Christopher alimshukuru Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, kwa namna ambavyo emeendelea kuwa msaada mkubwa katika shughuli zao, ikiwemo kuwapa ofisi mjini Tarime.

Aidha, aliwahimiza maafisa usafirishaji wenzake ambao hawajasoma udereva kuhakikisha wanakwenda kusoma taaluma hiyo kwenye vyuo vinavyotambulika serikalini, kikiwemo kile kinachomilikiwa na Professor Mwera Foundation.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages