MENEJA wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa, Sofia Mziray (katikati mbele) akisalimiana na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ekwabi Mujungu kabla ya kikao kuanza. |
MENEJA wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa, Sofia Mziray amesema bado kuna changamoto ya utunzaji wa kumbukumbu za dawa zenye madhara ya kulevya.
Mziray ameyasema hayo kwenye kikao kazi kilichowakutanisha watumishi wa sekta ya afya na mifugo ambacho kimefanyika kwa muda wa siku mbili (Mei 6 na 7, 2021) kuona namna ya kufanya shughuli za uthibiti, lengo likiwa kuona mkoa wa Simiyu na Kanda ya Ziwa kwa ujumla hakuna bidhaa zisizokuwa na ubora.
"Bado kuna changamoto kuanzia wanaponunua dawa hadi wanapohifadhia unakuta dawa tayari tumetengeneza mfumo ambao unatumia hadi simu za kawaida, yaani hata aliye kijijini ambaye hana smartphone anaweza kutumia mfumo huo kutoa taarifa, dhima ya TMDA ni kulinda afya za wananchi na suala la uthibiti si la taasisi pekee hata wananchi ni wadau wakubwa na huwa tunapata taarifa kwa wananchi.
"Na hizi dawa zenye madawa ya kulevya zisipotumika vizuri, zisiposimamiwa vizuri zinaweza kuleta madhara makubwa sana na tayari tumeweka mfumo wa kuzisimamia lakini bado kuna wenzetu wanaotunza dawa hizi bado kwingine kuna changamoto ya utunzaji, hivyo tumeona tukae pamoja kukumhushana na ni matumaini yetu maaimio ya kikao hiki yatafanyiwa kazi," amesema Mziray.
Sehemu ya washiriki wa kikao kazi hicho
Mziray amesema kwamba mara nyingi wakiwa kwenye ukaguzi wamekutana na dawa ambazo hazina ubora, bandia na ambazo hazijasajiliwa na kuongeza kuwa tayari TMDA imeweka wakaguzi ngazi ya mkoa ambao watasaidia kuthibiti hali hiyo.
Awali akifungua mafunzo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ekwabi Mujungu amesema kufanya kazi bila taarifa (kumbukumbu) ni tatizo kubwa ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka huku akiwataka kupitia kikao kazi hicho kuja na suluhisho la kudumu.
"Mnaohusika si lazima watu mpaka watoke Dar es Salaam kuja kuona dawa bandia fanyeni kazi kwa mujibu wa viapo vyenu,” amesema Mujungu.
Nao washiriki wa kikao hicho wamesema watayafanyia kazi yale yote yaliyoazimiwa na kuhakikisha jamii ina kingwa na madhara yanayoweza kuepukika.
(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)
No comments:
Post a Comment