NEWS

Monday 10 May 2021

Watoto zaidi ya 400,000 kupatiwa kingatiba SimiyuWashiriki wa kikao cha uraghibishi na uhamasishaji wa kingatiba mkoani Simiyu.

WATOTO zaidi 400,000 wenye umri wa kwenda shule watapatiwa kingatiba mkoani Simiyu ili kuwakinga na magonjwa ya kichocho na minyoo.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka mkoa wa Simiyu, Dkt Ntugwa Nyorobi wakati akiwasilisha mada kwenye kikao cha uraghibishi na uhamasishaji kilichofanyika Mei 7, 2021 kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki la mjini Bariadi.

"Tunatarajia kutoa kingatiba kwa watoto wenye umri wa kwenda shule, yaani kuanzia miaka mitano hadi 14 walioko shule na wasiokuwa shule 417,593 kwa mkoa mzima, lengo ni kuwakinga na kichocho na minyoo na tayari tumetengewa kiasi cha Shilingi milioni nane na elfu moja kwa ajili ya ufanikishaji wa zoezi hili," amesema Nyorobi.

Wahiriki wakifuatilia mada kikaoni

Naye Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka wilaya ya Busega, Nkwaya Shukia amesema maambukizi bado yapo juu ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2020 watoto waliokuwa na minyoo ni 4157 na kichocho ni 365.

"Mfano mzuri tulipima wanafunzi 600 kutoka kwenye shule 10, wanafunzi 156 walikuwa na kichocho na 56 walikuwa na minyoo," amesema Shukia.

Lucy Kulong'wa ni Afisa Elimu Wilaya ya Maswa, amesema ni bora kuanza na kisababishi cha magonjwa hayo kwa kudhibiti vyanzo vya maambukizi na kuongeza kuwa kutoa dawa kwa watoto pekee haitoshi, hivyo ameshauri uwepo mkakati wa kutoa kingatiba kwa jamii nzima.

Kwa upande wake, Programe Ofisa wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Isaac Njau amesema kiwango cha maambukizi ya magonjwa hayo katika Kanda ya Ziwa kiko juu ikilinganishwa na kanda nyingine.

Umakini ukiendelea kikaoni

Katika hatua nyingine, Kaimu Mratibu Mpango huo, Oscar Kaitaba amesema changamoto kubwa ipo maeneo ya vijijini na ambayo watu wanajishughulisha na kilimo cha kwenye majaruba na uvuvi na kufafanua kuwa ni rahisi mtu kupata kichocho endapo maji yatakuwa yana vimelea vya kichocho.

Awali akifungua kikao hicho, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema magonjwa ya kichocho na minyoo tumbo yanaongeza matumizi ya
rasilimali zilizopo na kwamba fedha zilizotengwa mkoani humo inapaswa zitumike kwa mujibu wa matarajio ili kuleta matokeo chanya.

(Habari na picha: Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages