NEWS

Thursday 17 June 2021

Bonge la Mpango NMB: Tarime yatoa mshindi
KWA mara ya kwanza, Benki ya NMB imemkabidhi mshindi wake wa kampeni ya Bonge la Mpango, Babyana Magori Mang’era, zawadi ya pikipiki ya mizigo aina ya LIFAN yenye thamani ya shilingi milioni 4.5.

Babyana ambaye ni mwalimu na mfanyabiashara ya mitumba mjini Tarime mkoani Mara, amekabidhiwa pikipiki hiyo na Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus leo Juni 17, 2021.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Benki ya NMB Tawi la Tarime, ambapo meneja huyo amemkabidhi Babyana pia kadi na bima ya pikipiki hiyo ya magurudumu matatu.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Ladislaus amempongeza Babyana kwa kuibuka mshindi wa kampeni ya Bonge la Mpango, iliyozinduliwa na Benki ya NMB Februari mwaka huu, kwa lengo la kurejesha faida kwa wateja wake na kuhamasisha utamaduni wa kujiwekea akiba kwa Watanzania.


Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus (kulia) akimpa Babyana kipaza sauti azungumze baada ya kukabidhiwa zawadi ya pikipiki ya mizigo. Kushoto ni Meneja wa NMB Tawi la Tarime, Victorine Roman Kimario na wafanyakazi wa benki hiyo.

Ladislaus amesema kampeni hiyo inahamsisha wateja wa Benki ya NMB kuweka na kutuma fedha kupitia akaunti zao, kuanzia shilingi 100,000.

“Kampeni ya Bonge la Mpango inawezesha wateja kushinda fedha taslimu, pikipiki za miguu mitatu aina ya LIFAN, magari ya kubeba mizigo maarufu kama Kirikuu aina ya TATA Ace na gari la kifahari aina ya Toyota Fortuner.

“Pia, kampeni hiyo imelenga kuwahamasisha wasio na akaunti ya benki nchini kuja kufungua na kutunza akiba zao kwa njia salama zaidi na benki ya NMB,” amesema Ladislaus.


Babyana akiendesha pikipiki hiyo

Kwa mujibu wa meneja huyo wa NMB Kanda ya Ziwa, mpaka sasa benki hiyo imeshatoa zawadi za fedha taslimu kwa washindi 120, pikipiki za mizigo aina ya LIFAN kwa washindi 24, magari madogo ya mizigo aina ya TATA Ace kwa washindi watatu na gari la kifahari aina ya Toyota Fortuner kwa mshindi wa kampeni ya Bonge la Mpango.

“Mpaka leo [Juni 17, 2021], zawadi zote hizi zina thamani ya shilingi zaidi ya milioni 294. Kikubwa zaidi leo tunatoa zawadi kwa mshindi wetu ambaye ni mkazi wa Tarime, Babyana Magori Mang’era aliyejinyakulia pikipiki ya mizigo aina ya LIFAN yenye thamani ya shilingi 4,500,000," amesema Ladislaus.Furaha ya zawadi

“Pia, tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kuhusu bidhaa na huduma mpya zinazotolewa na benki ya NMB, ikiwemo bima kwa wanavikundi - ambapo NMB ikishirikiuana na kampuni ya bima ya Metropolitan hutoa mkono wa pole pale mwanakikundi anapofariki dunia, au kufiwa na mwenzi, au mtoto wake,” ameongeza Ladislaus.

Ameongeza kuwa benki ya NMB pia inatoa huduma ya Mastaboda ambayo ni mikopo ya Bodaboda kwa wafanyabiashara wadogo.

“Najisikia furaha sana na nawashukuru wafanyakazi wa benki ya NMB kwanza kwa kunihasamisha kufungua akantii NMB na kwa kuanzisha kampeni ya Bonge la Mpango,” amesema Babyana na kutumia nafasi hiyo kuwahamisha wananchi wa Tarime kufungua akaunti na kutumia huduma za benki hiyo.


Babyana akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi yake ya pikipiki ya mizigo.

“Naomba mfungue akaunti NMB ili siku moja mpate zawadi kubwa kuzidi ya hii yangu,” Babyana amesisitiza.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages