NEWS

Monday 28 June 2021

BRAC yafikisha huduma za mikopo nafuu kwa wanawake Serengeti




KATIKA kutekeleza na dhamira yake ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini, BRAC Tanzania Finance Limited (BTFL) imezindua rasmi tawi lake katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Tawi hilo lililopo mjini Mugumu, limezinduliwa rasmi na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Serengeti, Cosmas Qamara.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na watendaji wa serikali za mitaa ya mji wa Mugumu na viongozi wa vikundi vya mikopo ya akinamama, Qamara ameipongez BTFL kwa kuifikia wilaya ya Serengeti kwa huduma za mikopo ili kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa akinamama wanaojikita katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Nawapongeza BRAC kwa hatua hii na ninafarijika kuona nia yenu ya kuwanyanyua wanawake kiuchumi. Napenda kuwashauri akinamama wanaopata fursa hii waitumie vizuri kwa kutumia mikopo kwa shughuli husika na kuirejesha kwa uaminifu ili na wengine waweze kupata.

“Vilevile ningependa kushauri shirika lifikirie kuleta mikopo ya wakulima ili na akinababa nao wapate fursa ya kuendeleza shughuli zao za kilimo. Serengeti ni wilaya yenye shughuli nyingi za kilimo na wakulima hawa pia wanahitaji huduma za kifedha,” ameongeza DAS huyo.


DAS Qamara akizungumza wakati wa uzinduzi wa BRAC Tawi la Serengeti

Kwa upande wake, Meneja wa BRAC Tanzania Finance Ltd Mkoa wa Mara, Eunice David amesema shirika hilo limejipanga kusaidia shughuli za kiuchumi za wakazi wa wilaya ya Serengeti, kupitia mikopo midogo midogo yenye masharti nafuu, hususan kwa wanawake ambao ndio walengwa wakuu wa shirika hilo.

“Wanawake ndio uti wa mgongo wa Taifa letu na hivyo tumejikita katika kuwawezesha kujikomboa kiuchumi. Huduma ya mikopo ya vikundi isiyokuwa na dhamana ndio bidhaa yetu kuu na imeundwa mahsusi kwa ajili ya wanawake wajasiriamali na wakulima, kwa sababu tunaelewa changamoto za wanawake katika kupata huduma za kifedha.

“Ni matumaini yetu kuwa kupitia mikopo hii, wanawake wa wilaya ya Serengeti wataweza kuwekeza katika shughuli zao za kiuchumi na hivyo kutimiza malengo yao kijamii na kiuchumi,” amesema Eunice.

“BRAC ni shirika kubwa zaidi nchini linalotoa huduma za kifedha ndogo ndogo nchini, ni shirika lililojikita katika kubadilisha maisha ya wateja wake kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.”

Shirika la BRAC linajivunia utoaji wa huduma jumuishi za kifedha kwa njia ambayo ni rahisi, kupitia bidhaa zilizoundwa kukidhi mahitaji ya wateja wake.


Baadhi ya wafanyakazi wa BRAC Tawi la Serengeti

Mkoani Mara, BRAC ilianza kutoa huduma mwaka 2008 katika mji wa Musoma ambako kuna matawi mawili, matawi mengine yapo katika wilaya za Tarime, Bunda na kuongezeka kwa tawi jipya la wilaya ya Serengeti, kunafanya shirika hilo kuwa na matawi matano mkoani humo.

BRAC inajivunia kuwa na matawi 155 yaliyopo katika wilaya 83 kwenye mikoa 23 kati ya 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar. BRAC pia inajivunia kuwa mshirika mkubwa kwa wanawake, kwani asilimia 97 ya wateja wake nchini ni wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo, wakulima na wafugaji.

Pamoja na mkopo usio na dhamana kupitia vikundi vya kinamama, BRAC pia hutoa huduma za mikopo binafsi kwa wanawake na wanaume wajasiriamali.

Dhamira ya BRAC ni kutoa huduma mbalimbali za kifedha kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu kiuchumi, hasa wanawake wanaoishi vijijini na maeneo ambayo upatikanaji wa huduma za kifedha ni mgumu. Lengo kuu ni kuwapatia fursa za kujiajiri, kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha na kuendeleza ndoto zao za ujasiriamali.

BTFL ni sehemu ya BRAC International, shirika la maendeleo ambalo ni sehemu ya shirika mama la BRAC lililoanzishwa nchini Bangladesh mwaka 1972 na Hayati Sir Fazle Hasan Abed. Kwa sasa BRAC inafanya kazi katika nchi 11 katika mabara ya Asia na Afrika.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages