NEWS

Wednesday 16 June 2021

IGP Sirro aonya wanaotoza faini wezi wa mifugo





MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amefanya ziara wilayani Tarime, Mara na kupiga marufuku vitendo vya viongozi wa mitaa na vijiji kuwatoza faini wezi wa mifugo na kuwapatanisha na walalamikaji.

“Habari ya kuiba na kukaa mnaelewana haina nafasi, mwenyekiti asishiriki kupatanisha wezi na kuwapiga faini,” IGP Sirro ameonya wakati akizungumza na viongozi wa mitaa, vijiji na jeshi la sungusungu mjini Tarime, leo Juni 16, 2021.

IGP Sirro amesisitiza kuwa hakuna kiongozi wa kijiji wala mtaa anayeruhusiwa kufanya majadiliano ya kuwalipisha faini wezi bila kuwafikisha mahakamani.

“Mwizi akikamatwa na ushahidi afikishwe mahakamani mara moja, ni kosa la jinai kuanza majadiliano naye, kiongozi atakayekutwa anamlipisha mwizi faini bila kumfikisha mahakamani, na yeye ataunganishwa kwenye kosa la wizi,” amesema IGP Sirro.

Aidha, amewataka viongozi wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime-Rorya, kuwapa ushirikiano viongozi wa serikali za mitaa na vijiji ili kukomesha uhalifu kwenye kanda hiyo.

“Polisi peke yao hawawezi kutokomeza uhalifu bila kusaidiana na hao, ukimuona mtendaji, au mwenyekiti wa kijiji anakuja ofisi kwako, kama ofisa wa polisi lazima umtambue kuwa ni kiongozi muhimu ili upate ushirikiano kutoka kwake,” amesema IGP huyo.


IGP Sirro akizungumza katika mkutano huo

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini amewaambia viongozi hao kuwambia wananchi wao kwamba uhalifu haulipi kwa sasa, kwani jeshi hilo lina uwezo wa kukabiliana na wahalifu sugu, ambao wamekuwa wakipelekwa mahakamani na kuachiwa.


RPC wa Tarime-Rorya, William Mkonda (aliyesimama) akitoa taarifa kwa IGP Sirro

Kwa upande wao, viongozi hao wamemweleza IGP Sirro kuwa matukio ya uhalifu yamepungua, ingawa kuna changamoto za polisi kuchelewa kufika kwenye matukio wanapoitwa, kutokana na ukosefu wa vyombo vya usafiri, jambo ambalo Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi amesema ataona namna ya kushughulikia tatizo hilo.

(Imeandikwa na Mobini Sarya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages