NEWS

Monday 14 June 2021

Mamilioni yahofiwa kufujwa Tarime Vijijini, Tume yaundwa kuchunguza kitengo cha manunuzi, wakandarasi waliorundikiwa miradi




TUME maalum imeundwa kwa ajili ya kuchunguza vitengo vya manunuzi, ukaguzi wa ndani wa fedha na wakandarasi waliorundikiwa miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), mkoani Mara.

Tume hiyo imeundwa na Mkuu wa Mkoa (RC), Mhandisi Robert Gabriel - siku chache kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko madogo ya wakuu wa mikoa na kumhamisha kutoka Mara kwenda Mwanza, Ijumaa iliyopita.

RC Gabriel amechukua hatua hiyo, baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kutilia mashaka baadhi ya matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

“Tumekagua, tumesikiliza ripoti nyingi, hapa kuna shida, kuna shida kwenye upande wa manunuzi, kuna shida kwenye upande wa usimamizi wa fedha, kuna shida kwenye upande wa ukaguzi wa ndani. Kuna fedha nyingi sana zimetolewa hapa.

“Ofisi yangu imeunda timu ya uchunguzi, kuangalia fedha yote iliyotolewa, nione thamani halisi ya fedha kwenye miradi. Hiyo fedha siyo zawadi ya mtu, hiyo fedha siyo ya mhandisi, au ya mkuu wa idara, ni fedha ya umma, na inatolewa, inasimamiwa kwa kanuni, taratibu na sheria za nchi,” RC Gabriel amesema katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa, ripoti ya CAG imebaini ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za matumizi ya fedha za umma katika halmashauri hiyo, inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Apoo Castro Tindwa.

“Ni fedha nyingi ambazo zimetumika bila utaratibu, na imeonekana kwamba nyaraka hazikai ofisini, nyaraka hii ukitaka inakosekana, nyaraka hii inakosekana, nyaraka inakosekana,

“Lakini pia, kuna mashaka Mkaguzi ameyaona kwenye baadhi ya matumizi ya fedha… menejimenti bado haijaleta majibu yenye kuridhisha. Nimeona pia comments (maoni) za madiwani wa kamati ya fedha zinasema kanuni, sheria na taratibu zizingatiwe, na kitengo cha manunuzi kiangaliwe.

“Kwa hiyo, mimi naondoka na hayo, kwamba timu yetu ya mkoa, mojawapo ya jambo kubwa la kufanya ni kuangalia hicho kitengo cha manunuzi kilichopo hapa, lazima tutende haki kwenye kujiridhisha. Waliosababisha hizo hoja na utata huo mkubwa, matumizi ambayo siyo rafiki - hayaeleweki, tutaomba tuwajue vizuri ni akina nani.

“Kwa hiyo, mahali ambapo fedha tutagundua imepotea, imepungua tutadai chenji, hiyo naomba niseme wazi, miradi iliyopita na ijayo, tutadai chenji yetu,” amesisitiza Mhandisi Gabriel.

Ameongeza kuwa tume aliyoiunda itamulika pia wakandarasi waliopewa zabuni za miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo, huku akiiagiza Mamala ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Tarime, kuwafuatilia ili kuona kama wamelipa ushuru wa huduma (service levy) na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mujibu wa sheria.

“Wakandarasi wengi mno wamepewa miradi mingi mno, lazima tuwajue, tujiridhishe kwamba wamelipa service levy - ushuru wa huduma wote. Lakini pia, nitoe agizo kwa TRA Tarime, wawajue wakandarasi wote kwenye hiyo miradi, wawe wamewalipa VAT,” RC Gabriel ameagiza na kuongeza:

“Dalili nyingi zinaonesha vitu vimekwenda kinyume kinyume, tunataka tuwekane vizuri, twende vizuri, maendeleo yetu yaende vizuri. Mimi changu kimoja tu, nitawasaidia watu wasiwaibie, na nataka tuanze na Tarime, tena halmashauri hii [Tarime Vijijini], nina maana yangu kwanini tuanze na hapa.”


RC Gabriel (katikati) akihutubia baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini). Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Victoria Mapesa na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Apoo Castro Tindwa.

RC Gabriel amewaahidi madiwani katika kikao hicho kwamba kamati aliyoiunda kuchunguza mambo hayo, itafanya kazi hiyo na kutoa ripoti yenye mapendekezo ndani ya muda mfupi.

Aidha, amebaini kuna haja ya kupeleka mafunzo ya kuwajengea madiwani uwezo wa kusimamia utendaji na maendeleo katika halmashauri hiyo, kwa manufaa ya wananchi.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Tarime (Vijijini) inaongoza kwa mapato makubwa mkoani Mara, hivyo inahitaji usimamizi thabiti unaojumuisha madiwani.

Miongoni mwa chanzo kikubwa cha mapato ya halmashauri hiyo ni Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ambao huipatia mabilioni ya fedha - zikiwemo za ushuru wa huduma kila mwaka.

“Nimefuatilia mapato kwenye kipindi hiki ambacho tunakaribia kufunga mwaka, nimepata zaidi ya bilioni tano za mapato ya ndani, na bado kuna utajiri mkubwa wa fedha ambazo zilikuwa na changamoto mbalimbali za matumizi, zaidi ya miaka miwili zimezuiliwa.

“Tunataka mtu akipita Tarime kwenye mitaa, akikosa kijani, aone majengo mazuri yenye hadhi, yakiwemo ya afya, elimu na miradi ya vijiji,” amesema RC huyo.

(Imeandikwa na Mana Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages