NEWS

Thursday, 10 June 2021

Mkoa wa Mara wazindua mkakati wa chakula kwa wanafunzi



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Robert Gabriel.

MKOA wa Mara umezindua mpango mkakati wa huduma ya chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari mkoani humo, kama njia ya kuinua kiwango cha taaluma na ufaulu.

Akizundua mkakati huo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Elimu yaliyofanyikia kimkoa wilayani Rorya hivi karibuni, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Saimon Odunga, amelipongeza Shirika la PCI kwa kufadhili mchakato wa kuandaa mkakati huo.

“Huu mpango mkakati ni nyenzo muhimu itakayosadia kuanza kugawa chakula na lishe katika shule zote na mkoa wa Mara utakuwa wa kwanza nchini, kutekeleza mpango wa chakula shuleni,” amesema Odunga.

DC Odunga (katikati) akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mpango mkakati huo.

Awali, Mkurugenzi wa Mradi wa PCI, Amina Mgeni amesema awali shirika hilo lilianza kugawa chakula shuleni katika baadhi ya halmashauri kama njia ya utafiti kwa awamu tatu.

“Kwanza tulianza mkakati huu kwa wilaya chache za mkoani hapa kugawa chakula shuleni, mradi uliokuwa wa awamu tatu zinazoishia Septemba mwaka huu, tumesaidia kupunguza utoro katika shule ambazo chakula kinatolewa,” amesema Amina.

Amina amesema mkakati huo unalenga kuhamasisha jamii kuchangia chakula kama PCI ilivyofanya na kwamba tayari tani zaidi ya 50 za chakula zimechangwa kwa ajili hiyo.


Amina Mgeni akizungumza katika uzinduzi huo

Shirika la PCI ambalo linafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Wizara ya Kilimo nchini humo, limekuwa likisaidia utekelezaji wa miradi katika wilaya za Bunda, Musoma na Butiama, limefanikiwa kujenga vyoo na maktaba, matenki ya maji na vyumba vya kubadilishia nguo katika shule mbalimbali mkoani Mara.

Aidha, PCI inatarajia kushirikiana na Wizara ya Elimu kuzindua mpango mkakati wa kitaifa, utakaosaidia kugawa chakula na lishe kwenye shule zote nchini.

Akizungumza kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya mkakati huo, Afisa Lishe wa Wilaya ya Bunda, January Dalushi amesema mkakati ni wa miaka mitano inayoishia mwaka 2025.

“Mpango huu umetoakana na kikao cha wadau, kilichofanayika Februarya 2020 mjini Musoma, kikabaini kuwa kukosekana kwa huduma ya chakula shuleni kunachangia utoro na kushusha kiwango cha ufaulu,” amesema Dalushi.

(Imeandikwa na Mobini Sarya, Rorya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages