
Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema (katikati), kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wilayani Rorya jana Jumatano wakati wa futari iliyoandaliwa na taasisi hiyo.
Rorya
--------------
Mamia ya wananchi, wengi wao wakiwa Waislamu wa wilayani Rorya, mkoani Mara, jana Jumatano walijitokeza kupata futari ya pamoja waliyoandaliwa na Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation - NF).
Mgeni rasmi katika hafla ya futari hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, aliwakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Boniface Chambi, ambaye aliipongeza taasisi hiyo kwa tendo hilo la upendo.
"Nyansaho Foundation amefanya jambo la maana, Tanzania ni moja - kama tunavyoona hapa tupo Waislamu na wasiokuwa Waislamu, inaonesha mshikamano wa kitaifa, hatubaguani kwa rangi, dini au kabila, ni jambo la upendo.
“Tudumishe umoja wa kitaifa, kila mmoja amlilie Mwenyezi Mungu ili nchi yetu idumishe umoja na mshikamano,” alisema Chambi na kuendelea:
"Baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na Kwaresima, nitoe wito kwa waumini wote wayaishi matendo mema ambayo wameyafanya katika mwezi huu mtukufu.”

Naye Sheikh wa Wilaya ya Rorya, Abubakhar Khamis, aliishukuru Taasisi ya Nyansaho na kutumia nafasi hiyo pia kuhimiza amani, mshikamano na upendo katika jamii.
"Nishukuru kwa futari hii kutoka Nyansaho Foundation. Nawahimiza Waislamu na wasiokuwa Waislamu kuendeleza umoja na amani, maana Ramadhani inakuja kama mwalimu.
“Katika maandiko Bwana Yesu alifunga siku 40 ambazo ndizo Wakristo wanatekeleza kama ambavyo tunafunga. Funga inatupa funzo kwa ajili ya kumnyenyekea Mola na kuwa na utulivu na amani kwa watu wengine,” Sheikh Khamis.

Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema (katikati), akiwa na viongozi wa dini wakati wa hafla hiyo ya futari.
Awali, Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, aliwashukuru waamini hao kwa mapokezi makubwa, huku akitaja shughuli muhimu za taasisi hiyo katika jamii.
"Tunashukuru sana kukubali tukio hili. Tunajihusisha na elimu, afya na mahitaji maalum kwa kutoa usaidizi kwa kaya duni ambazo zina changamoto katika kutatua matatizo waliyonayo kwa kuwaelekeza sehemu sahihi au sisi kuwasaidia.
"Wito wetu mkuu ni kuhakikisha tunakuwa raia wema katika taifa letu na kuwa wazalendo na kuwasaidia ndugu zetu wanapokuwa na changamoto. Unaposaidia Mwenyezi Mungu anakutakabari na kukubarikia zaidi,” alisema Modester.
Hivi karibuni, Taasisi ya Nyansaho pia iliandaa futari kama hiyo kwa siku tofauti kwa wananchi wa wilaya za Tarime, Musoma, Bunda na Serengeti, mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment