NEWS

Monday 14 June 2021

Rais Samia ahimiza utunzaji Ziwa Victoria, ulipaji bili za maji




RAIS Samia Suluhu Hassan amewahimiza wananchi kutunza miradi ya maji na vyanzo vyake, likiwemo Ziwa Victoria, kwa uendelevu na ubora wa huduma hiyo isiyo na mbadala katika jamii.

Sambamba na hilo, Rais Samia amewahimiza wananchi kuzingatia ulipaji wa bili za maji kwa wakati, ili kuwezesha mamlaka za maji kuendeleza na kuboresha usambazaji wa huduma hiyo kwa kiwango cha kuridhisha.

Amesisitiza hayo mara baada ya kuzindua mradi wa maji mjini Misungwi, Mwanza leo Juni 14, 2021, ambapo pia amewataka watumishi wa mamlaka za maji kuhakikisha hawabambikii wananchi bili za huduma hiyo.

“Tutunze hili Ziwa [Ziwa Victoria] na kuhakikisha vyanzo vingine vyote vinaendelea kumimina maji ndani ya ziwa hili,” Rais Samia amesema katika hotuba yake.


 

Rais ametahadharisha kuwa uharibifu wa vynazo vya maji unaweza kufifisha juhudi zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama nchini.

Kuhusu miradi ya maji, amesema serikali inatumia fedha nyingi zikiwemo za mikopo kuitekeleza, hivyo kila mwananchi ana jukumu la kuilinda na kuitunza idumu muda mrefu, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Aidha, Rais amewashauri wananchi kujenga utamaduni wa kuvuna maji ya mvua, ikiwa ni pamoja na kujenga malambo na mabwawa ili kupunguza kama si kumaliza tatizo la uhaba wa maji katika maeneo mengi nchini.

Mkuu huyo wa nchi amewashukuru washirika wa maendeleo walioipatia serikali mkopo wenye masharti nafuu, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji Misungwi.

Rais Samia ameiagiza mamlaka husika kutumia mradi huo kuharakisha usambazaji wa huduma ya maji, kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya wakazi wa mji huo.

Ametumia nafasi hiyo pia, kuitaka Wizara ya Maji kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji iliyobaki nchini, inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.


RAIS Samia (wa pili kulia) akizindua mradi wa maji Misungwi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemhakikishia Rais Samia kwamba yeye na wasaidizi wake wamejipanga kuongeza usimamizi ili kuona wananchi wanapata maji safi na salama, ikiwezekana kwa gharama nafuu zaidi.

Aidha, Waziri Aweso amesema ataendelea kuondoa wahandisi na makandarasi wababaishaji, akisisitiza kuwa watu wa aina hiyo hawana nafasi tena katika wizara hiyo.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga katika taarifa yake kwa Rais, amesema utekelezaji wa mradi wa maji Misungwi wenye uwezo wa lita milioni 4.5, umegharimu Sh bilioni 13.77 na utahudumia wananchi 64,000.

Mhandisi Sanga amesema kazi ya kuunganishia wananchi huduma ya maji ya mradi huo inaendelea chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWUWASA).

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages