NEWS

Sunday 13 June 2021

Rais Samia azindua kiwanda cha kusafisha dhahabu, jengo la BoT Kanda ya Ziwa
RAIS Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Madini na mamlaka husika nyingine serikalini, kuongeza udhibiti wa wizi na utoroshaji wa madini, kwani yana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ajira nchini.

Pia, ameagiza watendaji wa serikali ngazi za wilaya na mikoa kuhakikisha wachimbaji wadogo wanaendelea kutengewa maeneo maalumu, kuwezeshwa mafunzo na teknolojia waweze kuchimba kisasa na kwa tija.

Rais Samia ametoa maagizo hayo jijini Mwanza leo Juni 13, 2021, ambapo amezindua kiwanda chenye mtambo mkubwa zaidi Afrika Mashariki wa kusafisha dhahabu, na jengo la kisasa la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Kanda ya Ziwa.

Katika hotuba yake ya uzinduzi huo, Mkuu huyo wa nchi amesema kuna haja ya kuongeza usimamizi kuanzia kwenye migodi ya madini, yakiwemo ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee duniani.

Kuhusu Tanzanite, Rais Samia amesema “Kuna haja ya kuwa na mfumo wa kuidhibiti ili inunuliwe na mwamvuli mmoja wa mashirika yanayonunua Tanzanite na uuzaji wake. Waziri [wa Madini] kaa na wawekezaji husika muone mfumo mzuri wa kuilinda, kuidhibiti na kupandisha hadhi yake kwenye soko la dunia.”

Kwa upande wa wachimbaji wadogo, Rais amesema “Wachimbaji wadogo wasimamiwe vizuri wachimbe zaidi. Sekta ya madini inaajiri vijana wengi na kutupunguzia tatizo la ajira, wasaidiwe ili wajenge chumi zao, watunze familia zao.”

Rais Samia amesisitiza kuwa rasilimali za Tanzania lazima zitumike ipasavyo ili kuwaletea wananchi maendeleo, na ametaka mkwamo wa uchimbaji wa chuma katika maeneo ya Mchuchuma na Liganga utafutiwe ufumbuzi haraka, kazi iendelee.

“Mchuchuma na Liganga ifanye kazi, tuanze kuchimba sasa na itumike ndani, lakini pia tuuze nje,” amesema Rais Samia.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye sekta ya madini, akiwahakikishia kuwa Tanzania ni tajiri kwa madini ya aina nyingi - ikiwemo dhahabu, Tanzanite, chuma, fedha na almasi.

Akizungumzia kiwanda hicho chenye mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu, Rais Samia amesema kitakuza ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa, kutokana na uwezo wake wa kusafisha madini hayo kwa kiwango cha ubora wa asilimia 99.

“Mtambo [wa kiwanda hicho] utawezesha Benki Kuu ya Tanzania kununua dhahabu, utasaidia kuchochea uchimbaji wa madini na shughuli za kiuchumi jijini Mwanza,” ameongeza.

Rais amewataka wachimbaji wa madini kujipanga ili kuhakikisha kiwanda hicho kinapata mali ghafi ya kutosha, kwani kwa sasa kimeanza na uwezo wa kusafisha dhahabu hadi yenye uzito wa kilo 450 kwa siku.
 

Kiwanda hicho kimejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 12.2 na imeelezwa kitatoa ajira 120 za moja kwa moja na 400 zisizo za moja kwa moja kwa wananchi.

Awali, Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema mchango wa madini kwa pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia nne mwaka jana hadi 6.7 mwaka huu.

Uzinduzi wa BoT
Akihutubia wananchi katika kuzindua jengo la BoT Kanda ya Ziwa, ambalo ujenzi wake umegharimu Sh bilioni 40, Rais Samia ameipongeza benki hiyo kwa kudhibiti kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania na kuwezesha wananchi kutumia mifumo sahihi ya kifedha kwa asilimia 65.

Pia, ameipongeza BoT kwa kuimarisha usimamizi wa benki na taasisi nyingine za kifedha na kujenga uchumi wa nchi.


 

Hata hivyo, Rais Samia ameelezea kutofurahishwa na mikopo yenye masharti magumu, viwango vikubwa vya riba na muda mfupi inayotolewa na benki na taasisi ndogo za kifedha kwa wakopaji, akisema ni kikwazo cha ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa kawaida.

“Watanzania wengi wanashindwa kukopa kutokana na masharti magumu na viwango vikubwa vya riba. Kuna wakati mtu alikuwa anatakiwa kukopa kwa mfano, shilingi milioni moja na kutakiwa kulipa shilingi milioni moja na nusu kwa miezi sita,” amesema.

Ameitaka BoT kuchukua hatua za makusudi, kuhakikisha kuwa benki na taasisi ndogo za kifedha zinapunguza masharti na viwango vya riba ili kuwezesha wakopaji kukua kiuchumi.

“BoT angalieni suala hilo lisiwe kikwazo kwa wakopaji na wafanyabiashara. Naelekeza viwango vya riba vianze kushushwa, angalau viwe kwenye asilimia 10 kwenda chini, benki zitoe mikopo ya muda mrefu,” Rais Samia ameagiza.

Pamoaja na mafanikio ya kuwezesha huduma jumuishi, Rais ameitaka BoT kuhamasisha pia matumizi ya fedha kwa njia ya mtandao badala ya fedha taslimu, akisema utaratibu huo utapunguza gharama za uchapaji wa fedha mara kwa mara.

Rais Samia anaendelea na ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mwanza, ambapo kesho Jumatatu atakagua ujenzi wa Daraja la JPM (Kigongo-Busisi), kuzindua mradi wa maji Misungwi na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, eneo la Fella wilayani Misungwi.

Keshokutwa Jumanne, Rais atakutana na kuzungumza na vijana wa Tanzania kupitia kwa vijana wa Mwanza, kwenye uwanja wa Nyamagana.

(Imeandikwa na Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages