
Na Christopher Gamaina
Musoma
---------------




Musoma
---------------
Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC) wamejengewa uelewa wa majukumu na faida za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa wanachama na wastaafu.
Semina hiyo ya siku moja imefanyika leo Januari 22, 2026 mjini Musoma, ambapo pia wanahabari hao wameelimishwa matumizi na faida za PSSSF Portal na PSSSF Kiganjani.
Afisa Uhusiano Mwandamizi kutoka PSSSF Makao Makuu Dodoma, Rehema Mkamba, amesema wanaendesha semina za aina hiyo kuboresha uhusiano na wanahabari kwa ajili ya kusaidia kufikisha ujumbe kwa umma.
“Ni kawaida yetu kuendesha semina za aina hii kwa waandishi wa habari,” amesema Rehema wakati akifungua semina hiyo.

Kaimu Meneja wa PSSSF Mkoa wa Mara, Nuru Malinya, ametaja majukumu ya mfuko huo kuwa ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Nuru amebainisha kuwa PSSSF inajihusisha na mafao ya Uzeeni, Ulemavu na Mirathi, pamoja na mafao ya muda mfupi ya Uzazi, Ukosefu wa Ajira na Ugonjwa.
Aidha, ametaja faida za matumizi ya Portal PSSSF na PSSSF Kiganjani kuwa ni kufanya mambo kwa uwazi, kurahisisha huduma na kuepusha utapeli.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MRPC, Jacob Mugini, ameishukuru PSSSF na kuiomba kuendeleza semina za aina hiyo kwa waaandishi wa habari wa mkoani Mara.
“Naomba semina za aina hii ziwe endelevu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Sisi waandishi wa habari tuliopata semina hii tutakuwa mabalozi wazuri wa PSSSF kwa jamii,” amesema Mugini ambaye pia ni Mkurugenzi wa vyombo vya habari vya Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara.

Mwenyekiti huyo wa MRPC ametumia nafasi hiyo pia kuishauri PSSSF kuangalia uwezekano wa kuanzisha tuzo kwa waandishi wa habari nchini wanaofanya vizuri kwenye habari za mfuko huo.

No comments:
Post a Comment