Mhandisi Robert Gabriel
MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Mhandisi Robert Gabriel, amesema Halmashauri ya Mji wa Tarime inaweza kupanda kuwa Manispaa, ikiwa vyanzo vyake vya mapato vitasimamiwa vizuri.
RC Gabriel amebainisha hayo katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, cha kupitia hoja zilizoibuliwa kwenye taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mjini Tarime, leo Juni 7, 2021.
“Mimi bado ni mgeni katika mkoa huu, lakini nilipoingia Tarime nilibaini kuwa huu mji unapaswa kuwa Manispaa ndani ya muda mfupi kama vyanzo vya mapato yake vitabainishwa na kusimamiwa vizuri,” amesema Mhandisi Gabriel.
RC Gabriel (katikati) akizungumza katika kikao hicho. Kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa mfano wa mkataba wa kujenga vibanda kwenye soko la wakulima Rebu, ambao amesema halmashauri hiyo inapaswa kuupitia upya, kwani inapoteza mapato kizembe kwa kumwachia mwekezaji mapato makubwa.
“Mkataba kama ule wa ujenzi wa vibanda 54 pale sokoni, kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mkuu wa Wilaya iupitie upya. Huwezi kuwa na ardhi mjini unampa mtu, yeye anatoa milioni 200 na wewe unatoa tena milioni 48 kwa mkataba wa miaka 15, bado unamwachia ajisimamie kwenye gharama za ujenzi,” ameonya RC Gabriel.
Amesema ni kama halmashauri hiyo imegawa eneo hilo bure, kwani inaambulia Shilingi 20,000 kwa mwezi, wakati mwekezaji anapokea Shilingi 130,000 kwa kila kibanda, hivyo kuifanya halmshauri hiyo kukosa mapato makubwa ambayo yangeifanya ipige hatua kubwa kimaendeleo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri kutumia kamati yake ya ulinzi na usalama, kuwasaka watumishi hewa ‘waliotafuna’ mishahara ya halmashauri hiyo - Shilingi zaidi ya milion.24, bila kuripoti kazini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa (kushoto) akizungumza katika kikao hicho.
Naye Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote amesema ingawa wamejitahidi kuepuka hati chafu, madiwani wanaomba wapatiwe semina kuhusu namna ya kusimamia mikataba ya kisheria na manunuzi ili kupunguza upotevu wa mapato ya halmashauri hiyo.
“Tukipatiwa semina, hata hilo kablasha la CAG wakati mwingine litapungua kurasa, kutokana na hoja zinazoibuliwa, Madiwani tunaomba tupatiwe semina ya sheria na taratibu za manunuzi ili tuweze angalau kuwa na uelewa wa kisheria,” amesema Komote.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment