NEWS

Thursday 17 June 2021

Right to Play yahimiza ulinzi na utetezi haki za watoto

SHIRIKA la Right to Play limesisitiza kuwa ulinzi na utetezi wa haki za watoto ni jukumu la jamii nzima.

Mwezeshaji wa shirika hilo, Leah Kimaro ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika wilayani Serengeti, Mara yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Robanda, jana.

Leah amesema watoto wanastahili kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili, kuthaminiwa na kupewa haki zao ikiwemo ya elimu ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Siku ya Mtoto wa Afrika sisi mashirika tunaungana kwa sauti ya pamoja kupinga na kulaani vikali vitendo vya ukatili vinavyotokea kwenye jamii yetu, watoto ni tunu ya taifa, lazima tuwalinde, tuwathamini,” amesema Leah.


Leah (kulia) akikabidhi kombe kwa washindi wa michezo ya watoto siku hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Nyumba Salama Mugumu, Daniel Misoji amesema shirika hilo linaendelea kulinda na kutetea haki za watoto kwa kuhakikisha hawafanyiwi ukatili, ukiwemo wa kupigwa na kutelekezwa na jamii.

Misoji ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha wazazi kuhakikisha wanatimiza jukumu la malezi bora kwa watoto wao, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka bila ubaguzi wa kijinsia.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la WorlChanger Vision Serengeti, Sulus Samwel amesema maadili na makuzi bora ya watoto yako mikononi mwa wazazi na jamii kwa ujumla.

Mkazi wa kijiji cha Robanda, Bhoke Chacha amesema baadhi ya wazazi wameshindwa jukumu la malezi, hivyo kuna haja ya serikali kutunga sheria ya kuwabana wazazi na walezi wasiotimiza wajibu wao kwa watoto.


Mtoto akionesha kombe la ushindi siku hiyo

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Nurdin Babu amesema serikali inaendelea kusajili watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ili waweze kupatiwa vyeti vya kuzaliwa bure.

DC Babu amefafanua kuwa mpaka sasa watoto zaidi ya 70,000 wenye umri huo wamesajiliwa na kupewa vyeti bila malipo wilayani Serengeti.

“Serikali inatoa vyeti bure lakini kuna changamoto ya wazazi kutowapeleka watoto wapatiwe vyeti, mpaka wasubiri pale wanapopata nafasi za JKT na Polisi ndio wanajipanga ili kufuatilia vyeti, sasa nasisitiza wazazi wachangamkie fursa hiyo,” amesema Babu.


DC Babu akihutubia wakati wa maadhimisho hayo

Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza mpango mkakati wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya mama na mtoto, ikiwemo kujenga mazingira mazuri kwa watoto, usalama na stadi za maisha shuleni.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema “Tutekeleze Ajenda 2040: kwa Afrika Inayolinda Haki za Watoto”.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages