NEWS

Sunday 6 June 2021

Shirika la FZS laadhimisha Siku ya Mazingira Duniani Kwa kuwezesha mafunzo ya mpango ya matumizi ya ardhi



Meneja Mradi wa FZS, Masegeri Rurai

SHIRIKA la uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) Tanzania, limeadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kuwezesha mafunzo ya kuanzisha Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika vijiji vya Bokore na Nyichoka wilayani Serengeti, Mara.

“Kwa kuwa mipango ya matumizi ya ardhi inasaidia kutunza mazingira, tumeona pia ni jambo zuri kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyo jirani na ikolojia ya Serengeti,” Meneja Mradi wa FZS, Masegeri Rurai amesema.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa Juni 5 kila mwaka, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu inasema “Tutumie Nishati Mbadala: Kuokoa Mfumo wa Ikolojia”.

Akizungumzia mafunzo ya mpango wa matumizi ya ardhi, Masegeri amesema vijiji vya Bokore, Nyichoka, Rwamchanga na Kazi viko katika mchakato wa kuanzisha mpango huo kwa uwezesho wa shirika hilo.


Wananchi wakishiriki mafunzo hayo kijijini Bokore

“Hadi sasa tumeshaandaa mpango wa matumizi ya ardhi katika vijiji 18, sasa hivi tunaendelea na vijiji vingine vinne (ili kukamilisha vijiji 22 vya wilayani Serengeti).

“Lengo kubwa la kuandaa hii mipango ni kuwezesha wananchi kumiliki ardhi yao, Lakini kikubwa pia ni kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, kwa sababu hivi vijiji vyote vinapakana na maendeo ya hifadhi,” amesema Masegeri na kuendelea:

“Ardhi ikipangiliwa vizuri, kwa mfano maeneo ambayo ni mapito ya wanyamapori kama tembo, tunawashauri wasilime mashamba, wayaweke kwa ajili ya malisho - mifugo inachunga mchana, lakini hata wanyamapori wakija wanaweza wakapita. Hapo unakuwa umepunguza mgogoro kati ya wanyamapori na binadamu.

“Pia mradi huu unawezesha kuwapa wananchi hatimiliki za ardhi [za kimila]. Hizi hati ni muhimu kwa ajili ya umilikishaji wananchi ardhi zao, na mwananchi anapopata zile hati maana yake ni kwamba wanaweza kutumia katika kujiendeleza kiuchumi.

“Kwa mfano, wanaweza kuzitumia hata kuchukua mkopo benki kwa ajili ya kufanya biashara, au hata kupanua maeneo yao ya uwekezaji, kwa mfano kilimo, huduma za jamii na kadhalika,” amesema Masegeri ambaye ni mpenzi wa uhifadhi wa wanyamapori.

“Kwa ujumla shughuli hizi za matumizi ya ardhi ni katika kutekeleza sera ya serikali, na hapa tunashirikiana kwa karibu na TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania), lakini pia Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kupitia Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi,” amebainisha.


Sehemu nyingine ya washiriki wa mafunzo hayo

Masegeri amesema wataalamu wa Tume hiyo wanasaidiana na wataalamu wa Halmshauri ya Wilaya ya Serengeti kuhakikisha kazi hiyo inafanywa vizuri kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi.

“Mradi huu tunautekeleza kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW), ndio wanatupatia fedha kwa Serikali ya Tanzania. Sisi Shirika la Frankfurt Zoological Society kwa kushirikiana na TANAPA ndio tunatekeleza mradi huu,” Masegeri amebainisha.

“Lakini pia mpango wa matumizi ya ardhi pia unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha na kuhifadhi mazingira. Tunaamini kwamba kwa kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji, kunasaidia kuboresha na kuokoa ikolojia ya Serengeti.

“Kwa sababu kupitia mipango ya matumizi bora ya ardhi, wananchi wanatenga maeneo ya misitu, mapito ya wanyama, ardhi oevu na upandaji miti,” amesema Masegeri.

Kwa mujibu wa Mtaalamu Mshauri wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi kutoka FZS Tanzania, Christopher Cuthbert, vijiji vilivyowezeshwa kuanzisha mpango huo na kutenga maeneo ya shughuli mbalimbali, huandaliwa mabango ya ramani inayoonesha mgawanyo wa maeneo na mengine yanayoonesha matumizi ya kila eneo, lakini pia alama za mipaka ya maeneo husika.

“Tunasimamia kuhakikisha wanavijiji wanatengenezewa mpango wa matumizi ya ardhi, na tunawaandalia mabango maalumu ya kuwasaidia kutambua matumizi ya kila eneo. Mpango huu unasaidia kutunza na kuhifadhi mazingira yao na ikolojia ya Serengeti kwa ujumla,” amesema Cuthbert.


Christopher Cuthbert akizungumza na Mara Online News

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mipango Miji na Vijiji kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Christopher Kazeri, ametaja faida nyingine ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi kuwa ni kuwezesha wanavijiji kuwa na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.


Christopher Kazeri akielezea faida za mpango wa matumizi ya ardhi

Mkazi wa kijiji cha Bokore, Nyambura Mturi ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo ya uanzishaji wa mpango wa matumizi ya ardhi kijijini hapo, ana matumaini makubwa ya kunufaika na mpango huo.

Nyambura ambaye ni moja ya wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Bokore wanaopata mafunzo na kushiriki kundaa mpango huo anasema “Kwa sisi wanawake mpango huu utatusadia kujua mipaka ya wanyamapori na maeneo yetu, tutafanya shughuli zetu kwa amani, kwa sababu wanyamapori pia wanafika kwenye vyanzo vya maji.”


Nyambura Mturi akizungumza na Mara Online News kijijini Bokore

“Tunaamini kwamba mpango huu utatusaidia pia kulinda na kutunza vyanzo vya maji,” amesema Nyambura na kuungwa mkono na mwanakijiji mwenzake, Nyabitara Chagina ambaye ana shauku ya kuona mpango huo unawezesha upimaji wa ardhi zao na utengaji wa maeneo ya malisho ya mifugo kijijini hapo.

Nyabitara anaamini kwamba mpango huo utawasadia pia kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki. “Tunatamani kuanza kufuga nyuki na pia kupata visima vya maji,” anasema mwanamke huyo ambaye naye anashiriki katika maandalizi ya mpango wa matumizi ya ardhi katika kijiji cha Bokore.

Viongozi wa ngazi ya kijiji na kata katika eneo hilo wameelezea kuridhishwa kwao na mwitikio wa wananchi kwenye mpango wa matumizi ya ardhi.

Viongozi hao, wakiwemo Diwani wa Kata ya Kyambahi, Herman Kinyariri, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bokore, Juma Wambura na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Mwita Wambura, wamesema uhamasishaji wa mpango huo umekuwa mkubwa kuanzia kwenye uundaji wa kamati ya usimamizi wa ardhi na baraza la ardhi la kijiji.

Mwenyekiti Wambura anasema ukosefu wa mipaka ya maeneo muhimu ndani ya kijiji hicho ni chanzo cha migogoro. “Hali hii inasababisha shida ya tembo, simba na fisi kuvambia maeneo ya wananchi na kuwepo kwa migogoro mingi kijijini,” anasema.


Mwenyekiti Wambura akielezea shauku yake juu ya mpango wa matumizi ya ardhi kijijini Bokore

Diwani Kinyariri anafurahi kuona kuwa vijiji vyote vya kata yake vimeingizwa kwenye mpango wa matumizi ya ardhi.

“Mfano, Bokore sasa kitakuwa mwanachama wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Ikona na kuanza kupata mgao wa mapato, maana ili kijiji kiwe ndani ya WMA, lazima kiwe na mpango wa matumizi ya ardhi.

“Wananchi wasiwe na wasiwasi, waiamini serikali yao na serikali za vijiji, kwani mpango huu unapitishwa na mikutano mikuu ya vijiji,” anasema Kinyariri na kuhakikishia wananchi kuwa mpango huo una lengo zuri la kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.


Diwani Kinyariri akizungumza na Mara Online News kijijini Bokore

Raha ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi
Bwitengi ni miongoni mwa vijiji 18 vilivyokwisha kuanzisha mpango wa matumizi ya ardhi wilayani Serengeti.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Raphael Marere ameieleza Mara Online News kwamba mpango huo umekuwa suluhisho la migogoro baina ya wafugaji na wakulima, na kwa upande mwingine, wanamapori na binadamu katika kijiji hicho.

“Sasa hivi kila mwananchi anafurahia utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji chetu. Wananchi wanaheshimu maeneo yaliyotengwa, migogoro kati ya wakulima na wafugaji iliyokuwepo imekwisha, sasa hivi wakulima na wafugaji hawaingiliani.

“Tumetenga maeneo ya kilimo, malisho, huduma za jamii, barabara, misitu, uwekezaji, makaburi na vyanzo vya maji, kila mwananchi anaheshimu mpango huu,” anasema Marere.


Mwenyekiti Marere akielezea furaha yake juu ya mpango wa matumizi ya ardhi ulioanzishwa kijijini Bwitengi

Naye mkazi wa kijiji cha Bwitengi, Daniel Nyamronga ametaja mambo yaliyopokewa kwa furaha kubwa kutokana na mpango wa matumizi ya ardhi kuwa ni pamoja na utengaji wa maeneo ya njia za mifugo kijijini hapo.


Nyamronga akionesha bango linaloonesha eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo kijijini Bwitengi

Mchakato unavyofanyika
Mtaalamu Mshauri wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kutoka Shirika la FZS, Cuthbert, amesema uanzishaji wa mipango hiyo katika vjiji hivyo unafuata sheria zote husika, huku chombo cha uamuzi katika ngazi ya kijiji kikiwa ni Halmashauri ya Serikali ya Kijiji.


Christopher Cuthbert akionesha bango linaloonesha utengaji wa maeneo kwa ajili ya shuguli tofauti kijijini Bwitengi

Afisa Mipango Miji na Vijiji kutoka TAMISEMI, Kazeri, anayeshiriki kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, anasema wataalamu kutoka idara mbalimbali za halmashauri kama vile ardhi, wanyamapori, mazingira, sheria na misitu wanashirikishwa kikamilifu katka mchato huo.

“Lakini wenye maamuzi makubwa katika kuandaa mipango hii ni wananchi wenyewe. Sisi kazi yetu ni kuelekeza,” anasema Kazeri ambaye pia ni mtaalamu wa mazingira.

Amefafanua kuwa shughuli ya kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi unaweza unachukua wastani wa siku 10 hadi siku 14.

Kazeri anaongeza kuwa wajumbe wa baraza la ardhi la kijiji na kamati ya usimamizi wa ardhi ya kijiji wanashikiri katika mchato wa awali wa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ambapo wanapewa elimu ya kutosha kuhusu aridhi, usimamizi wa mazingirana na rasilimali zake.

Anataja moja ya sheria zinazozingitiwa katika uandaaji wa mpango huo kuwa ni Sheria Namba 6 ya Mwaka 2007.

Utelekezaji wa mpango huo unaenda sawia na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, ambayo inaelekeza serikali kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji zaidi ya 4,000 nchini kwa mwaka 2020/2025, kwa muijibu wa mtalaamu huyo wa mipango miji na vijiji.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages