NEWS

Monday 7 June 2021

JATU yazindua kampeni ya Buku Tano, hii fursa si ya kukosa





KAMPUNI ya JATU (JATU PLC) imezindua kampeni ya ‘Buku Tano’, inayompa mwananchi fursa ya kuwa mwekezaji katika kampuni hiyo, kwa kununua hisa 10 kwa bei ya Shilingi 5,000.

JATU PLC imezindua kampeni hiyo katika viwanja vya Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Juni 5, 2021.
Kutoka kushoto ni wajumbe wa Bodi ya JATU Saccos Ltd, Mariam Mrutu, Gregory Imbele, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Isare Gasaya, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo, Dkt Mhandisi Zaipuna Yonah na Phinias Opanga, wakizindua uuzaji wa awali wa hisa za JATU PLC jijini Dar es Salaam, juzi. Uzinduzi huo uliambatana na Kaulimbiu inayosema "Buku Tano Inatosha".

Aidha, JATU PLC imetangaza mchakato wa kuingiza hisa mpya sokoni, kwa ajili ya wawekezaji wapya wa ndani na nje ya Tanzania, huku wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wakitakiwa kuchangamkia fursa hiyo, kupitia tawi la kampuni hiyo lililopo kwenye jengo la Olympic jijini Mwanza.



JATU PLC imetangaza fursa hiyo baada ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), kuidhinisha waraka wa matarajio ya kampuni hiyo, kwa ajili ya kuuza kwa umma hisa, katika soko la awali.

Kwa mujibu wa taarifa ya JATU PLC kwa umma, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Peter Isare Gasaya, Juni 3, 2021, CMSA imeidhinisha waraka huo Mei 31, 2021.



CMSA imeidhinisha waraka huo wa JATU PLC chini ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania).

Taarifa hiyo inafafanua kuwa, JATU PLC inatarajia kuuza hisa 15,000,000 kwa bei ya Shilingi 500 kwa kila hisa.



“Hisa hizo zinauzwa kuanzia Juni 1, 2021 mpaka Julai 15, 2021 na zitaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Julai 29, 2021,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ya JATU PLC na kuendelea:

“Katika kipindi cha mauzo ya hisa hizo katika soko la awali, uuzaji wa hisa za JATU PLC kwenye soko la upili (DSE), utasimama hadi Julai 28, 2021 (siku moja kabla ya kuorodheshwa kwa hisa mpya).



“Kwa mantiki hiyo, uuzaji wa hisa za JATU PLC katika DSE utaendelea kuanzia Julai 29, 2021 baada ya kuorodheshwa kwa hisa mpya za JATU PLC.”

Waraka wa matarajio wa JATU PLC unapatikana katika tovuti ya kampuni hiyo (htps//www.jatu.co.tz) na kwa washauri wa uwekezaji na watendaji wa Soko la Hisa (brokers/dealers) walioidhinishwa na CMSA.



“Hisa hizi zote zinauzwa kwa wawekezaji wa Tanzania na wa nje ya Tanzania; wenye rika na jinsia zote, ikiwa ni pamoja na wanawake, wanaume, watoto, vijana na watu wazima; watu wenye ulemavu; waishio mijini na vijijini,” imefafanua taarifa hiyo.

Kampuni ya JATU pia ina mradi wa kuanzisha kiwanda cha kusindika ndizi katika wilaya ya Tarime mkoani Mara na Super Market kubwa ya bidhaa mbalimbali jijini Mwanza.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages