NEWS

Thursday 17 June 2021

Siku ya mnada wa kimataifa Magena yatangazwa





HATIMAYE siku rasmi ya kufungua mnada wa kimataifa wa mifugo Magena uliopo Tarime mkoani Mara, imetangazwa kuwa ni Julai 22, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote ameiambia Mara Online News mjini Tarime jana Juni 16, 2021 kwamba maandalizi ya kufungua mnada huo ambao utakuwa ukifanyika kila Alhamisi yanaendelea kwa kasi.

“Ninavyozungumza na wewe tinga tinga lipo eneo la mnada linachonga barabara za kuingia na kutoka mnadani, wakati huo maofisa ardhi wapo eneo hilo wakichora ramani namna vibanda vitakavyojengwa,” amesema Komote.
Waziri Ndaki (katikati) siku alipokwenda kutangaza ufunguzi wa mnada wa Magena. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara na Mwenyekiti Komote (kushoto).

Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa za biashara wakati watakapotangaza kugawa viwanja katika eneo la mnada huo uliokuwa umefungwa kwa miaka zaidi ya 10.

Amesema kinachochelewesha mnada huo ni ukosefu wa miundombinu muhimu kama choo na ofisi, ambayo utekelezaji wake utaanza baada ya kupokea shilingi mililioni 150 walizoahidiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki.

Juni 12, mwaka huu, Waziri Ndaki alitembelea eneo hilo na kuidhinisha ufunguliwe tena huku akitoa siku saba kufikia leo Alhamisi Juni 17, siku ya ufunguzi iwe imejulikana.

“Nimekuja hapa kufungua mnada wetu wa Magena, naelekeza watendaji wangu wakae na Halmashauri watangaze siku rasmi ya mnada utakuwa inafanyika lini, ikifika Alhamisi Juni 17, mwaka huu niwe nimepata taarifa rasmi,” aliagiza Waziri Ndaki.

(Imeandaliwa na Mobini Sarya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages