NEWS

Monday 21 June 2021

Sote tuwe marafiki wa mazingira – Rais Samia




RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuwa marafiki wa mazingira kwa kuyatunza, vikiwemo vyanzo vya maji, kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.

Aidha, Rais Samia ametahadharisha kuwa mazingira yasipotunzwa yanaweza kugeuka kuadhibu binadamu, akitolea mfano kukauka kwa vyanzo vya maji.

“Mnapoyaudhi mazingira, yatakuadhibu mpaka urudi uwe rafiki yake,” amesema Rais Samia wakati akizungumza na vijana wa Kanda ya Ziwa siku yake ya mwisho ya ziara ya siku tatu mkoani Mwanza, hivi karibuni. “Niwaombe sana vijana, viongozi wa mkoa, tutunze mazingira,” amesisitiza.


Rais Samia akihutubia vijana jijini Mwanza

Rais ametaja baadhi ya mambo yanayochangia kuharibu mazingira kuwa ni ukataji wa miti na kuchoma misitu na hivyo kuchangia vyanzo vya maji kukauka. Amesema takwimwi zilizopo kuhusu upatikanaji wa maji wakati nchi inapata uhuru na sasa zinaonesha kupungua kwa kiasi kikubwa.

“Tulipopata uhuru wakati ule tulikwa watu milioni 10, kila mtu alikuwa na uwezo au na share yake ya maji, kila mtu lita 12,600, lakini leo tupo Watanzania karibu milioni 60, lita zetu za ujazo kwa mtu ni karibu 2,250, tukienda na hali tuliyonayo, lita hizi zinazidi kupungua, mwisho tutakuwa hatuna maji,” amesema.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa nchi ametaka uwekezaji mkubwa utakaobadilisha takwimu hizo, ambao utatoa fursa kwa kila binadamu anayezaliwa Tanzania kupata huduma ya maji.

“Kwa hiyo niwaombe sana, takwimu hizi hazitoi sura nzuri, twendeni tukarekebishe mazingira ili takwimu zetu zijibadilishe, tuongeze kiwango cha upatikanaji wa maji kwa kila binadamu anayezaliwa Tanzania,” amesema.

Pia, Rais Samia amehimiza wananchi kutunza miradi ya maji na vyanzo vyake, likiwemo Ziwa Victoria, kwa uendelevu na ubora wa huduma hiyo isiyo na mbadala katika jamii.

“Tutunze hili ziwa na kuhakikisha vyanzo vingine vyote vinaendelea kumimina maji ndani ya ziwa hili,” Rais Samia amesema muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa maji mjini Misungwi.


Sehemu ya Ziwa Victoria jijini Mwanza

Sambamba na hilo, Rais Samia amewahimiza wananchi kuzingatia ulipaji wa bili za maji kwa wakati, kuwezesha mamlaka za maji kuendeleza na kuboresha usambazaji wa huduma hiyo kwa kiwango cha kuridhisha.

Lakini pia, Rais Samia amewataka watumishi wa mamlaka za maji kuhakikisha hawabambikii wananchi bili za huduma hiyo.

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imekuwa ikitoa elimu ya kuhifadhi na kutunza ziwa hilo na vyanzo vyake, ukiwemo mto Mara.

Wakati huo huo, Rais Samia amesema serikali itaanzisha benki ya wajasiriamali kwa ajili ya mipoko kwa vijana, na kwamba itaendelea kuelekeza fursa mbalimbali kwa kundi hilo nchini.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages