IDADI ya tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeongezeka kutoka 6,000 mwaka 2014 hadi zaidi ya 7,000 mwaka 2020, kwa mujibu wa Taarisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
“Nyati nao wameongezeka kutoka zaidi ya 50,000 mwaka 2014 hadi 60,100 mwaka 2020,” Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Serengeti (SWRC), Dkt Robert Fyumagwa ameiambia Mara Online News katika mahojiano maalumu hifadhini humo, hivi karibuni.
Dkt Robert Fyumagwa
Dkt Fyumagwa amesema takwimu hizo, ni kwa mujibu wa sensa ya wanyamapori iliyofanywa katika hifadhi hiyo, Juni 2020.
Amesema ongezeko la wanyamapori hao, ni matunda ya juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha udhibiti wa vitendo vya ujangili.
Kwamba, mbinu mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia, imesadia kukabiliana na vitendo vya ujangili na biashara ya meno ya tembo, hivyo kuondoa tishio la kupungua kwa idadi ya wanyamapori hao.
“Ujangili kwa ajili ya meno ya tembo sio tatizo tena, ila kuna tatizo la kiimani,” amesema Dkt Fyumagwa ambaye ni Mtafiti Mwaandamizi wa TAWIRI.
Nyati ndani ya Serengeti
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Masana Mwishawa, amesema kuimarishwa kwa ulinzi kumesadia kuongezeka kwa idadi ya tembo katika hifadhi hiyo, ambayo ni sehemu ya urithi wa dunia.
“Sasa kinachotakiwa ni mipaka ya uhifadhi kuheshimiwa na kuelekeza nguvu katika mpango wa matumizi bora ya aridhi,” amesema Mhifadhi Mwishawa.
Mpango wa matumizi ya ardhi, unatajwa kuwa suluhisho la wanyamapori ambao wamekuwa wakivamia vijiji na kuharibu mazao ya chakula mashambani.
Wahifadhi wanasisitiza umuhimu wa kulinda na kutunza hifadhi hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo, kutokana na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti - Edeni ya Afrika
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ndiyo hifadhi bora Afrika, inatambulika kama eden ya Afrika, sehemu ya urithi wa dunia na ustiri wa maisha, na ni miongoni mwa Maajabu Mapya Saba ya Dunia.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment