NEWS

Monday 21 June 2021

Tunaomba tulindwe ili tutimize ndoto zetu - Wasichana wa Hope for Girls




WASICHANA walionusurika kufanyiwa vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji katika wilaya ya Serengeti, wameomba jamii kuheshimu haki za watoto waweze kufikia ndoto zao kielimu.

Wameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya kijijini Robanda, hivi karibuni.

Wasichana hao ambao kwa sasa wanafadhiliwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT), wameshukuru shirika hilo na serikali kwa kuwanusuru dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo vingeweza kukatisha ndoto zao.

“Tunachotaka ni haki zetu ili tuweze kufikia ndoto zetu, tuna ndoto nyingi na kubwa,” amesisitiza Rhobi Mwita kwa niaba ya wasichana wenzake, ambao kwa sasa wanapata huduma mbalimbali katika kituo cha Mugumu Nyumba Salama kinachoendeshwa na Shirika la HGWT.

Wasichana wanaosaidiwa kufikia ndoto zao wakitoa ujumbe kwa njia ya wimbo wakati wa maadhimisho hayo.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti (kabla ya kuhamishiwa wilaya ya Longido), Nurdin Babu amesema vituo vya nyumba salama vya shirika hilo vimekuwa kimbilio la wasichana wengi wanaokuwa katika mazingira hatari ya kufanyiwa ukatalii wa kijinsia kama vile kulazimishwa kukeketwa na kuolewa.

Vituo hivyo ni Mugumu Nyumba Salama na Butiama Nyumbaa Salama ambavyo vinaendeshwa na Shirika la HGWT.

“Nawapongeza sana wadau wa haki za watoto, mfano Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, kwa kuendelea kuhifadhi idadi kubwa ya watoto ambao wanakimbia ukatilii,” amesema DC Babu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.


DC Babu akihutubia maadhimisho hayo

Shirika la HGWT limetumia fursa hiyo kupasa sauti kuhusu umuhimu wa kulinda haki za watoto katika jamii, kwa njia mbalimbali ikiwemo mabango na nyimbo.

“Tunapasa sauti kuhusu kulinda na kuheshimu haki za watoto, tunataka jamii ijue kuwa mtoto ana haki ya kusikilizwa, kupata elimu, kucheza na hata kutoa mawazo kwa ajili ya ustawi wa jamii,” amesema Meneja wa kituo cha Mugumu Nyumba Salama, Daniel Misoji.

Misoji amesema mbali na kuhifadhi wasichana wanaokimbia ukeketaji na vitendo vingine vya kikatilii, shirika hilo limekuwa likitoa elimu vijijini kuhusu madhara ya ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni.

“Tunasisitiza kuwa mtoto, hususan wa kike, asigeuzwe kuwa mtaji kwa kuozeshwa mapema, au kufanyishwa kazi kwa lengo la kipato,” amesema Misoji.

Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16 kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema “Tutekeleze Ajenda 2040: kwa Afrikal Inayolinda Haki za Watoto”.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages