NEWS

Tuesday 29 June 2021

Wafahamu waliopewa simu janja kupiga vita ukatili wa kijinsia Tarime
SHIRIKA Lisilo la Kiserikali la ATFGM Masanga limegawa simu janja 210 zenye thamani ya Sh milioni 24.4, kwa mabalozi wa kupiga vita vitendo vya ukatilii wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike na wanawake, katika wilaya za Tarime na Butiama mkoani Mara.

Waliopewa simu hizo hivi karibuni, ni maofisa wa kitengo cha Intelijensia cha Polisi, maofisa watendaji wa kata na wananchi wa kawaida katika jamii, waliowezeshwa mafunzo maalumu ya kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao.

“Lengo hasa ni kutumia mtandao kuondoa hofu ya kulipiziwa kisasi kwa watoa taarifa,” Meneja Mradi wa Shirika la ATFGM Masanga, Valerian Mgani ameiambia Mara Online News katika mahojiano maalumu mjini Tarime, juzi.

“Simu hizi vimewekewa bando za internet za mwaka na zina aplikesheni mbili ambazo ni MPs-ME ambayo inaonesha eneo (location) na kila kitu kilichopo. Aplikesheni nyingine inajulikana kama Collect Organized Data Kit (ODK), ambayo ni kwa ajili ya kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa ATFGM Masanga, kitengo cha Itelijensia cha Polisi na Ustawi wa Jamii.

“Mtu akishapewa taarifa anaenda moja kwa moja hadi eneo la tukio bila kupata usaidizi wa mtu. Hii ni teknolojia ya hali ya juu na ina usiri mkubwa, lengo ni kumlinda mtoa taarifa,” amesema Mgani na kuongeza “Tuna imani hawa tuliowachagua ni watu sahihi, watatusaidia kutoa taarifa na zitafanyiwa kazi kwa njia sahihi.”


Valerian Mgani akionesha simu janja hizo

Mpango huo unalenga la kupungunza kama si kukomesha matukio ya ukeketaji, ndoa na mbimba za utotoni - ambvyo pia huchangia utoro kwa wanafunzi wa kike na hata kuacha shule.

Mgani amesema pango huo umefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) Tanzania, kwa lengo la kuimarisha mapambano dhdhi ya vitendo vya ukatilii wa kijinisa mkoani Mara, hususan katika wilaya za Tarime na Butiama - ambapo pia ATFGM kwa kushirkina na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT), wamegawa simu janja 59 kwa mabalozi wa kupiga ukatili huo.

Shirika la ATFGM Masanga limekuwa likitekeleza mipango na kampeni mbalimbali zenye lengo la kuwezesha wasichana wa kike kufikia ndoto zao kielimu na kupunguza ukatilii wa kijinsia katika wilaya ya Tarime, tangu mwaka 2008 lilipoanzishwa.

Hadi sasa shirika hilo limeweza kuokoa wasichana zaidi ya 3,000 waliokuwa katika mazingira hatari ya kufanyiwa ukeketaji na kuozwa katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Tarime na maeneo mengine ndani na nje ya mkoa wa Mara.

Lakini pia, ATFGM Masanga limesadia idadi kubwa ya wasichana kuhitimu elimu ya sekondari, vyuo na ngazi nyingine za elimu kwa lengo la kuwawezesha kufikia ndoto zao.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages