
Makamu Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Jafari Wambura Chege.
Uamuzi wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumchagua Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara, Jafari Wambura Chege, kuwa Makamu Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ni ishara ya imani kubwa waliyonayo juu ya uwezo, weledi na rekodi yake ya uongozi.
Hakika hatua hiyo siyo bahati nasibu, bali ni matokeo ya safari ndefu ya utendaji thabiti, kujituma bila kuchoka na uwajibikaji mahiri ambao umemjengea Chege heshima ndani na nje ya Bunge.
Mbunge huyo wa Rorya kwa tiketi ya chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni mfano wa kiongozi anayechanganya maono, vitendo na maadili, lakini pia anayeelewa kwa kina majukumu ya uwakilishi na usimamizi wa maslahi ya wananchi.
Chege ana weledi katika kujenga hoja zenye mashiko ndani ya Bunge, akichambua kwa umakini masuala yanayogusa maendeleo ya wananchi, hususan katika sekta zinazosimamiwa na TAMISEMI - kama elimu, afya, miundombinu ya barabara za vijijini, maji na uendeshaji wa serikali za mitaa.
Kama tujuavyo, TAMISEMI ni kamati nyeti katika Bunge, kwani inatokana na wizara mama inayogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania walio wengi. Hivyo, kumchagua Chege kuwa Makamu Mwenyekiti ni kuweka mtu sahihi mahali sahihi.
Uzoefu wake katika kusimamia hoja za maendeleo, uwezo wake wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya serikali na msimamo wake wa kusisitiza uwajibikaji kwa watendaji wa umma vinampa nafasi kubwa ya kuwa chachu ya ufanisi zaidi ndani ya kamati hiyo.
Katika mazingira ya kisiasa yanayohitaji viongozi wenye misingi imara ya maadili, Chege amejijengea taswira ya kiongozi asiyeogopa kusema ukweli, kusimamia haki na kusukuma mbele maslahi mapana ya wananchi bila kuyumbishwa na maslahi binafsi.
Huo ni mtaji mkubwa ndani ya kamati inayopaswa kuisimamia serikali katika ngazi za mikoa na halmashauri, ambako changamoto za kiutendaji na kiusimamizi mara nyingi hujitokeza.
Kama kiongozi mahiri, Chege ameonesha uwezo wa kufanya kazi kwa bidii ndani na nje ya Bunge. Jimbo la Rorya ni shahidi wa juhudi zake katika kusukuma maendeleo ya kisekta, akihakikisha kuwa sera na mipango ya serikali inawafikia kikamilifu wananchi wa kawaida.
Uzoefu huo wa moja kwa moja kutoka jimboni unampa Chege uelewa mpana wa changamoto halisi zinazokabili halmashauri na serikali za mitaa, jambo litakalomwezesha kuwa na mchango wa maana zaidi katika mijadala na maamuzi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI.
Naam, kwa mtazamo wa uchambuzi, uteuzi wa Jafari Wambura Chege katika nafasi hiyo unatarajiwa kuimarisha zaidi ufanisi, uwajibikaji na matokeo chanya ya kamati hiyo.
Ni matarajio ya wengi kwamba atatumia nafasi yake kusaidiana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Florent Kyombo, kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kutoa hoja zenye tija na kuhakikisha rasilimali za umma zinawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Chege anabeba matumaini mapya ya kuifanya kamati hiyo kuwa injini imara ya kusukuma mbele maendeleo ya wananchi kupitia serikali za mitaa.
Huu ni wakati wa kuthibitisha zaidi kile ambacho tayari amekionesha; kwamba uongozi bora ni ule unaojengwa juu ya utendaji thabiti, moyo wa kujituma, kuchapa kazi, uaminifu na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote ile.
Kila la heri Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Wambura Chege, katika utekelezaji wa majukumu yako mapya ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI.
No comments:
Post a Comment