NEWS

Monday 28 June 2021

Wanawake Anglikana Dar wasimulia raha ya kulala kwenye mahema Hifadhi ya Serengeti




HAIJAWAHI kutokea. Wanawake 200 kutoka Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, wameweka historia kwa kufanya utalii wa ndani, kulala kwenye mahema na kujionea wanyamapori mbalimbali wakiwemo simba, chui, pundamilia, kiboko, tembo, twiga na nyati mubashara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Wakizunguza na Mara Online News katika kambi ya mahema ya wageni eneo la Nguchiro hifadhini humo juzi, wanawake hao wamesema ni mara yao ya kwanza kutembelea hifadhi hiyo na wamefurahia vivutio vilivyomo, kuanzia kulala kwenye mahema hadi kutazama maajabu ya Mungu, yaani wanyamapori wa aina tofauti na uoto wa asili.


Wakiimba wimbo wa kusifia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

“Tumekuwa tukiona wazungu tu wanalala ndani ya mahema kwenye camp sites, lakini leo tumelala Watanzania, tena wanawake wa Dar es Salaam,” amesema mmoja wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Grace.

Mwanamke mwingine, Helena Charles ambaye ni mtumishi mstaafu amesema Serengeti ni hifadhi ambayo kila Mtanzania hapaswi kukosa kuitembelea ili kujionea aina mbalimbali za wanyama na uasili wa kuvutia.

“Mimi nimefurahi sana kufika Serengeti na nitatumia sehemu ya pesa zangu za kustaafu kuwaleta wajukuu wangu hapa Serengeti,” amesema Helena, akiwa ndani ya hema alimolala.


Kulala kwenye hema kumbe raha hivyo

Kwa upande wake, Sarah Hilary amesema Serengeti ni hifadhi yake ya tatu kutembelea baada ya Ngorongoro na Saadani. “Ndoto yangu ni kutembelea hifadhi zote 26 nchini kuona uumbaji wa Mungu na zawadi aliyotupatia, wanyama wazuri. Ni mara yangu ya kwanza kulala kwenye hema, stress (msongo wa mawazo) imetoka, tumenyoosha migongo, hakika Serengeti ni pazuri sana,” amesema.

Naye Meijini Mwamfumu amesema “Nimetembelea mbuga nyingi za hapa Tanzania, lakini Serengeti ni mara yangu ya kwanza, nimefurahi kuanzia njiani, tumeona uoto wa asili, tumelala kwenye tents (mahema), nime- experience kitu kizuri kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kulala kwenye tent."


Mojawapo ya picha za pamoja hifadhini

“Maisha hapa [Serengeti] yamekuwa mazuri, tumefurahi na asubuhi tumeamka tukiwa na nguvu vizuri, ninashukuru kwamba Serengeti wamejipanga vizuri kwa upande wa mapokezi na taratibu zao zote.

“Ninatoa wito kwa wamama wengine kwenye taasisi za kidini na zisizo za kidini, wamama binafsi kwenye familia, ni jambo zuri kujali vya kwetu, ni vizuri kama wanamama, kama familia, hata taasisi binafsi kutembelea hifadhi zetu ili kuona vivutio mbalimbali na kujifunza mengi, lakini pia kutangaza utalii wa ndani ya nchi yetu,” amesema Mwamfumu.


Mtoto Joan amefuatana na mama yake (kulia) katika utalii huo wa ndani

Viongozi wa hifadhi wanena

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Masana Mwishawa ameelezea kufurahishwa na ujio wa wanawake hao, akisema watakuwa mabalozi wa kuitangaza hifadhi hiyo na vivutio vyake.

“Wanawake hawa wamekuwa kundi la kwanza kubwa kutoka mikoa ya mbali, wameamua kulala kwenye mahema ili wapate vionjo tofauti na wanavyokuwa wanalala vyumbani kwao kwenye majumba na maghorofa makubwa,” amesema Mwishawa na kuendelea:

“Nchi kama South Africa (Afrika Kusini) inategemea watalii wa ndani kwa asilimia 90, sisi tunategemea watalii wa nje, sasa tubadilike tuweze kujikita kwenye utalii wa ndani, hatimaye tuendelee kupata watalii wengi wa ndani kutoka mikoa mbalimbali, sehemu hii ni muhimu zaidi kwenye pato la Taifa kwa ajili ya maendeleo.”


Mhifadhi Mwishawa akigawa zawadi kwa wanawake hao

Mwishawa amesema hifadhi hiyo ina uwezo wa kupokea na kuhudumia watalii wa ndani hadi 3,000 na kusisitiza kuwa gharama kwa watalii wa ndani ni nafuu ikilinganishwa na watalii kutoka nje ya Tanzania.

Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindaga George amesema mahema ni moja ya aina za malazi kwa ajili ya watalii zinazopatikana hifadhini humo na kubainisha kuwa gharama ya kulala kwenye hema ni shilingi 5,900 kwa kila mtalii wa ndani.


Mhifadhi Tutindiga (kulia) akiteta jambo na baadhi ya wanawake hao

“Tunahamasisha makundi mbalimbali ya watalii kutumia mahema, kwani ni sehemu tulivu na zinazovutia, kuna huduma zote muhimu kama maji na jiko. Wanawake hawa wameonesha mfano mzuri, kwani utalii wa kulala kwenye mahema ulikuwa wa wazungu, lakini hawa wanawake wamedhihirisha kuwa hata Watanzania wanaweza.

“Hii ni faraja kubwa sana kwetu (Hifadhi ya Serengeti) na tunategemea makundi mengine makubwa zaidi yatahamasika kutembelea hifadhi za Taifa. Hifadhi ya Serengeti inazo camp sites, hosteli na hoteli za kutosha na kuna maeneo ya malazi ambayo ni mazuri kwa shilingi 25,000,” amesema Tutindiga.


Pundamilia wameonekana mubashara hifadhini

Tutindiga amesema Hifadhi ya Taifa ya Serengeti chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), inaendelea kuhamasisha makundi mbalimbali ya wananchi kujitokeza kutembelea hifadhi hiyo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Safari ya ushirika huo wa wanawake wa Kanisa Anglikana Doyosisi ya Dar es Salaam, imeratibitwa na kufanikishwa na kampuni ya Land Africa Safaris, ambayo inatajwa kuwa ni mabingwa wa kubuni huduma mbalimbali za utalii wa ndani chini.


Simba wamekuwa kivutio kikubwa cha utalii Serengeti

“Huu ni utalii wa ndani na moja ya zao letu la utalii wa ndani, tunatarajia kuwa hawa wamama watakuwa mabalozi kwa makundi mengine kutembelea Hifadhi ya Serengeti,” amesema Mkurugenzi wa Land Africa Safaris, Timothy Mdinka.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages