NEWS

Wednesday, 14 January 2026

Mawaziri wapya Makonda, Katambi na wengine waapishwa, Rais Samia awapa maagizo



Viongozi mbalimbali walioteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni wakila kiapo Ikulu, Chamwino, jijini Dodoma jana.

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
-------------

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Mabalozi.

Hafla ya tukio hilo ilifanyika Ikulu, Chamwino jijini Dodoma, Januari 13, 2026, ambapo Paul Makonda aliapishwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku Patrobas Katambi akiapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.


Rais Samia akimuapisha Waziri Makonda


Waziri Katambi akila kiapo mbele ya Rais Samia

Wengine walioapishwa ni pamoja na Dennis Londo kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Ayoub Mohamed Mahmoud kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Richard Muyungi kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Mhandisi Zena Ahmed Said kuwa Balozi.


Balozi Zena akila kiapo

Rais Samia alisema mabadiliko ya uongozi ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa kuboresha utendaji wa serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, na kwamba uteuzi wa viongozi hao umezingatia uwezo, uzoefu, uadilifu na rekodi nzuri waliyonayo katika utumishi wa umma.

Alisema uteuzi wa Prof. Palamagamba Kabudi katika nafasi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Ikulu (Kazi Maalum) umetokana na uzoefu wake mpana, ukomavu wa kiuongozi na uelewa wa kina wa masuala ya Taifa, akibainisha kuwa dhamana hiyo inalenga kuimarisha ushauri na majukumu ya kimkakati ya serikali.

Aliwapongeza viongozi wote walioteuliwa na kuwasihi wakatimize majukumu yao kwa kuzingatia viapo vyao, na kuwataka kutekeleza kwa wakati ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.


Rais Samia akizungumza katika hafla hiyo

Akitoa maelekezo mahsusi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, Rais Samia aLImtaka kusimamia maandalizi ya Mashindano ya AFCON 2027 ambayo Tanzania ni mwenyeji, sambamba na kukuza vipaji vya wanamichezo vijana na kutumia michezo kama chombo cha ajira na umoja wa kitaifa.

Aidha, alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, kuimarisha amani, utulivu na mshikamano wa Taifa pamoja na kulinda misingi ya haki, utawala wa sheria na imani ya wananchi kwa serikali, na kuongeza kuwa wizara hiyo ina jukumu nyeti la kusimamia usalama wa raia na mali zao.

Rais Samia pia alisema uteuzi wa Dkt. Richard Muyungi katika nafasi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) unalenga kuimarisha uratibu wa sera za nchi katika kukabiliana na changamoto kwenye ajenda ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wa Mabalozi wapya, aliwataka kutambua dhamana waliyonayo ya kuwakilisha na kulinda heshima ya Tanzania kimataifa katika nchi walizopangiwa, sambamba na kutetea maslahi ya Taifa na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.

Rais Samia alihitimisha kwa kuwataka viongozi walioapa kufanya kazi kwa bidii, weledi na uzalendo, akiwakumbusha kuwa wamebeba matarajio makubwa ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages