NEWS

Sunday 13 June 2021

Ufunguzi mnada wa Magena: Waitara ataka wezi wa ng’ombe washughulikiwe





NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amewataka wakazi wa wilaya ya Tarime mkoani Mara kuhakikisha wanakomesha wizi wa ng’ombe, bila kuwaonea huruma watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijni, ametoa tamko hilo jana Juni 12, 2021 wakati wa ufunguzi wa mnada wa kimataifa wa mifugo katika eneo la Magena, nje kidogo ya mji wa Tarime.

Mnada huo ulikuwa umefungwa kwa miaka zaidi ya 10 kwa sababu za kiusalama.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Magena katani Nkende wakiwa kwenye miundombinu ya mnada huo.

“Najua ninavyoongea wezi hao wapo hapa hapa wananisikia. Nawashauri wananchi mchangamkie fursa za biashara, lakini msiwaache wezi wa mifugo wachafue sifa za mnada huu, mkiwakamata malizaneni nao huko huko wala msiniambie nitume rambirambi,” amesema Waitara.

Akifunga mnada huo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema wizara yake itatoa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kugharimia matengenezo ya miundombinu mbalimbali ya mnada huo.

“Nimekuja hapa leo kufungua mnada wetu wa Magena, naelekeza watendaji wangu wakae na Halmashauri watangaze siku rasmi ya mnada utakuwa unafanyika lini, ikifika Alhamisi Juni 17, mwaka huu niwe nimepata taarifa rasmi,” ameagiza Waziri Ndaki.

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Magena. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara.

Aidha, amewatahadharisha viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kutoweka tozo nyingi za ushuru ambazo zinaweza kuwa mzigo kwa wafanyabiashara na kuwafanya kukimbia mnada huo.

Ndaki ameitaka pia halmashauri hiyo kutumia mapato ya ndani kugharimia matengenezo ya barabara zinazoelekea kwenye mnada huo wenye eneo lenye ukubwa wa ekari 100, ili kuwezesha magari makubwa kuingia.

Wakati huo huo, Waitara amekabidhi magari mawili; moja la wagongwa na jingine kwa ajili ya idara ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

(Habari na picha: Mobini Sarya, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages