NEWS

Thursday 22 July 2021

Kanisa la AICT-MUD wahamasisha wazazi kuwapa watoto wa kike elimu bora




KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na taasisi ya Right to Play, limehamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutoa fursa sawa ya elimu bora kwa watoto, wakiwemo wa kike na wenye mahitaji maalumu.
 
Hayo yameelezwa Julai 22, 2021 wakati wa mashindano ya michezo mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la nne wa shule za msingi Nyansincha, Nyantira na Muringi zilizopo kata ya Nyansincha wilayani Tarime, yaliyoandaliwa kupitia mradi unaosimamiwa na kanisa hilo, unaolenga kuongeza ubora wa elimu na elimu jumuishi.


Mashindano yakiendelea

Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Afisa Mradi huo, Rebeca Bugota amesisitiza kuwa watu wote katika jamii wana wajibu wa kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wa kike na wenye mahitaji maalumu wanapata fursa sawa, ikiwemo ya elimu bora.

“Tunalenga kuhamasisha jamii kwa njia ya michezo itambue umuhimu wa kuwapatia watoto wa kike na wenye mahitaji maalumu elimu bora, hivyo wazazi wana wajibu wa kushiriki kuboresha elimu kwa watoto wao,” Rebeca amesema.


Rebeca akikabidhi kombe kwa timu ya Nyansincha iliyoishinda Nyantira kwa mabao 2-1.

Amebainisha kuwa mradi huo ambao unatekelezwa katika kata za Nyansincha, Itiryo na Nyamwaga, unawalenga wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza hadi la nne, ukijumuisha jamii, walimu na wadau wa elimu, ikiwa ni pamoja na kutenga vituo vya kusomea kila Jumanne na Alhamisi jioni.

Naye Afisa Elimu Kata ya Nyansincha, Mwalimu Sophia Range amelishukru kanisa hilo kwa kutekeleza mradi huo katika kata hiyo na kuwashauri wazazi na jamii kwa ujumla kuunga mkono, ili kuboresha elimu na kuwezesha watoto wa kike na wenye mahitaji maalumu kunufaika na fursa hiyo.


Mwalimu Sophia akihamasisha elimu bora kwa watoto

“Nawashukuru AICT kutekeleza mradi huu katika kata yangu, nawambieni wazazi bila kushirikiana na walimu, ubora wa elimu hauwezi kuonekana, kwani katika kata hii mahudhurio ya watoto shuleni ni mabovu,” Mwalimu Sophia amesema.



(Habari na picha zote: Mobini Sarya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages