
Na Mwandishi Wetu
Tarime
----------


Tarime
----------
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameagiza uongozi wa mgodi wa wachimbaji wadogo wa dhahabu Matongo uliopo kijiji cha Nyabichune, Nyamongo kudhibiti utiririshaji wa maji yenye kemikali za sumu kwenye mto Kwibeko.
Aidha, ameitaka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kufanya vipimo kwenye maeneo yanayozunguka mgodi huo na kutoa majibu, kwa usalama wa maisha ya watu na viumbe hai wengine.
DC Gowele alitoa maelekezo hayo Jumatano, Desemba 17, 2025 alipokwenda kukagua mgodi huo unaodaiwa kutiririsha kemikali za sumu kwenye mto Kwibeko na kusababisha vifo vya viumbe hai, wakiwemo samaki na vyura.

"Kwa sababu ya mashaka, wananchi kuona kitendo cha viumbe hai wamekufa, chura na samaki, lazima tujiulize maswali kwanini wamekufa, wakati huo maji hayo yanaendelea kutumika katika matumizi ya binadamu.
"Watu wa Bonde la Maji mmepima vipimo ambavyo vimeonesha mashaka – maana yake hapa pana changamoto, seneti zimo zinaonekana kwa macho, mnahitaji vipimo zaidi, hatuwezi kukubali wananchi waendelee kuathirika kwenye haya maeneo.
"Natoa siku tatu, watu wa Bonde ninyi ni watu wa serikali, chukueni vipimo kwenye maeneo yote tuletee hayo majibu… kipaumbele ni wananchi na maisha yao. Ili kuwa na uzalishaji wenye tija lazima haya mashaka tuyatoe,” aliagiza DC Gowele
Sambamba na hayo, DC Gowele ambaye aliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, aliutaka uongozi wa mgodi huo wa Matongo kufanya marekebisho ya miundombinu ya uzalishaji ili kuhakikisha usalama wa wananchi wanaoishi jirani.

DC Gowele akikagua bwawa la maji taka na kutoa maelekezo katika mgodi huo
"Muendelee kuboresha, ifikapo tarehe 20, Desemba [mwaka huu], tupate majibu yafike kwenye ofisi yetu ili tutoe maelekezo, kama litatokea tatizo hatutakubali muendelee kuzalisha,” alisisitiza.
Aliendelea: "Watu wa mgodi tusubiri majibu kutoka watu wa Bonde watuletee hivyo vipimo vikubwa tuone tutoe mashaka, vipimo vyao vimeonesha mashaka kwamba pana changamoto ya 'chemical', ninyi mnasema mmepima, tutajitahidi tuchukue majibu kutoka taasisi ya serikali.”
Abednego Erasto Msigala ambaye ni mtaalamu wa maji juu ya ardhi kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, alisema: "Sisi kama taasisi tumeyapokea maelekezo ya DC kwamba baada ya siku tatu tuwe tayari tumeleta taarifa kamili ya hali ya maji machafu kwenye huu mgodi.
Kwa upande wake Afisa Utawala Mgodi wa Dhahabu wa Matongo, Wulstan Muhonda, alisema: "Tumepokea mapendekezo yaliyotolewa na DC na tunaahidi kuyafanyia kazi yote na tuko tayari kupokea taarifa ya tarehe 20.”
No comments:
Post a Comment