NEWS

Wednesday 14 July 2021

BRELA yatwaa ushindi Maonesho ya Kimataifa ya Biashara

Washiriki wa Maonesho ya Sabasaba kutoka BRELA katika picha ya pamoja, baada ya kupata cheti cha ushindi wa tatu katika kundi la kuwezasha biashara na uwekezaji

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeng’ara katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yaliyofikia tamati jana Julai 13, 2021 katika Uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Katika maonesho hayo, BRELA imeibuka mshindi wa tatu katika kundi la washiriki wa maonesho, wanaojihusisha na uwezeshaji biashara na uwekezaji.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa washindi wa tatu, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema ushindi huo ni chachu ya kuboresha huduma na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.


CEO wa BRELA, Godfrey Nyaisa akionesha kombe la ushindi huo, baada ya kukabidhiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla



“Kwa sasa tunajiandaa na mpango wa kuwafikia wadau wetu waliopo katika mikoa 16, huu ukiwa ni mwendelezo wa zoezi la kuwafikia wateja wetu popote pale walipo," amefafanua Nyaisa.

Ameongeza kuwa BRELA imeshatoa elimu katika mikoa ya Njombe Singida, Ruvuma, Dodoma, Iringa na Morogoro, kwa lengo la kuwafikia wadau katika maeneo yao na kuwahamasisha kuhusu urasimishaji wa biashara na kufanya usajili wa papo kwa papo.


Maafisa Usajili wa BRELA wakiendelea kutoa huduma hiyo kwa wateja kwenye banda lao

Tangu kuanza kwa maonesho hayo Juni 28, 2021, BRELA imekuwa ikikutana na wadau wake na kuwatatulia changamoto zao papo kwa hapo na kutoa elimu kuhusu huduma zake, kuwahamasisha wadau mbalimbali kurasimisha biashara zao.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano BRELA, Roida Andusamile, ameeleza kwamba katika siku 16 za maonesho hayo, zaidi ya watu 1,000 walifika kwenye banda lao na kupatiwa elimu za papo kwa papo.


Mkuu wa Kitengo cha Habari na Elimu kwa Umma BRELA, Roida Andusamile (kushoto) akitoa elimu kwa mwananchi aliyefika kwenye banda lao la maonesho, kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo

“Wadau waliojiandikisha kufika katika mabanda yetu ni 1,200 na kati ya hao, 618 walipatiwa huduma za papo kwa papo za usajili wa majina ya biashara, kapuni, leseni za biashara kundi A na alama za biashara, pia wengine walipata elimu kuhusu huduma zetu na ushauri,” amesema Andusamile.


Ofisa leseni wa BRELA, Rehema Kionaumela (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja wa wananchi waliofika kwenye banda lao na kufanya usajili wa papo hapo wa jina la biashara na kupata leseni yake, wakati wa maonesho hayo ya Sabasaba

Maonesho hayo yalizinduliwa rasmi Julai 5, 2021 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tanzania, Dkt Philip Isdor Mpango na kufungwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

(Habari na picha: Mwandishi Wetu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages