NEWS

Sunday 25 July 2021

Hifadhi ya Serengeti yapokea kundi kubwa la watalii wa ndani kutoka Tarime, akiwemo Mkuu wa Wilaya



KWA mara ya kwanza, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, leo Julai 25, 2021 imepokea kundi kubwa la watalii wa ndani - zaidi ya 60 kutoka wilaya ya Tarime mkoani Mara, akiwemo Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Col. Michael Mtenjele.



Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Utalii wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Kanda ya Magharibi, Neema Mollel (kushoto mbele) akiwakaribisha watalii wa ndani na kuwapa maelekezo ya kitalii hifadhini.

Viongozi wa hifadhi hiyo wamepokea watalii hao kupitia lango la Lamai wilayani Tarime, kisha kuwatembeza kwa magari maalumu hifadhini, ambapo wamepata fursa ya kujionea mbashara wanyamapori mbalimbali, yakiwemo makundi ya nyumbu, simba, tembo, kiboko, mamba na pundamilia.



Sehemu ya makundi ya nyumbu yaliyowavutia zaidi watalii hao wa ndani



Watalii hao wa ndani pia wameshuhudia makundi ya viboko katika mto Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Watalii hao wa ndani wameeleza kuvutiwa mno na wanyamapori na mazingira hai ya hifadhi hiyo, ambapo pia wamepata fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu na watalii wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali.

Baadhi ya watalii wa ndani kutoka Tarime wakifurahia kukutana na watalii wa kigeni katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.


“Mimi ninashindwa kuielezea furaha yangu, nitarudi kuitembelea [Hifashi ya Serengeti] tena na tena na tena,” amesisitiza mmoja wa watalii hao wa ndani kutoka Tarime, aliyejitambulisha kwa jina la Thabita.



Hapa pia wakipata maelekezo ya mhifadhi

Miongoni mwa wahifadhi waliowapokea na kuwaongoza watalii hao wa ndani ni Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Utalii wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Kanda ya Magharibi, Neema Mollel na Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindaga George.

Wahifadhi hao wamewapongeza watalii hao kwa uamuzi wa kutembelea hifadhi hiyo ambayo ni kivutio bora Afrika, na kuwaomba wawe mabalozi wa kuitangaza kwa wananchi wengine.


Naye DC Mtenjele amewapongeza watalii wa ndani wenzake, wakiwemo waliokwenda na watoto, akisema hatua hiyo inawajenga hata watoto hao kuwa wazalendo na mabalozi wa kutangaza utalii wa ndani kwa Watanzania wengine.



Baadhi ya magari yaliyotumiwa na watalii hao wa ndani hifadhini

Safari hiyo ya watalii wa ndani kutoka Tarime, iliyopewa jina la “kuwapokea nyumbu Serengeti”, imehamasishwa na kuratibiwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa kushirikiana na taasisi ya Mara Online, Goldland Hotel & Tours na Taasisi ya Kizalendo Tanzania (TPO). Kaulimbiu ya safari hiyo inasema “Wanyamapori Wetu, Utalii Wetu”.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Col. Michael Mtenjele akionesha kibao cha lango la Lamai, kabla ya kuungana na watalii wengine wa ndani kutembelea hifadhi hiyo.
 

Habari zaidi kuhusu safari ya watalii hao wa ndani kutoka Tarime, itachapishwa kwa kina katika gazeti la Sauti ya Mara, toleo la kesho Jumatatu Julai 26, 2021.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages