NEWS

Tuesday 6 July 2021

Kiwanda cha Northern Highlands Coffee kilivyoongeza thamani ya zao la kahawa Tarime




KAHAWA aina ya Arabica inayozalishwa katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, imegeuka kuwa dhahabu nyeusi, baada ya bei yake kupanda mara dufu msimu uliopita.

Taarifa kutoka kwa wakulima na serikalini zinasema bei ya kahawa mbivu imepanda kutoka Sh 600 hadi 1,000 kwa kilo moja, huku bei ya kavu ikipanda kutoka Sh 1,200 hadi 1,400 kwa kilo moja.

“Pia wakulima wamelipwa malipo ya pili kwa msimu wa 2021 kwa shilingi 400 kwa kilo, jamabo ambalo halijawahi kutokea,” Afisa Kahawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime vijijini, Stanley Rubalila ameiambia Mara Online News mjini Tarime, hivi karibuni.


Kahawa iliyozalishwa na kiwanda cha Northern Highlands Coffee Company kilichopo Tarime ikiwa tayari kwa kunywa/ matumizi

Kupanda kwa bei ya kahawa kumesababisha wakulima wengi kuhitaji miche ya zao hilo la biashara kwa ajili ya kupanda.

“Sasa kuna hitaji kubwa la miche ya kahawa baada ya kahawa kugeuka kuwa deal, yaani ni dhahabu nyeusi,” amesema Rubalila.

Amesema halmashauri hiyo imepanga kugawa miche zaidi ya 200,000 kwa wakulima mara tu mvua za vuli zitakaponza.

Uwepo wa kiwanda cha kuzalisha na kufungasha kahawa cha Northern Highlands Coffee Company, kumeongeza thamani ya zao hilo ambalo ni tegemeo la mamia ya wakulima katika wilaya ya Tarime na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa.


Meneja wa Northern Highlands Coffee Company Limited, Rishit Radia (kulia) akimkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kahawa wanaoyozalisha - ikiwa tayari kwa matumizi, katika maonesho ya uzinduzi wa Muongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mara, uliofanyika mjini Musoma, hivi karibuni.

“sisi lengo la letu ni kuongeza thamani ya kahawa ili kunufaisha wakulima na kuendeleza sekta ya kilimo cha kahawa,” Meneja wa Kiwanda hicho, Rishit Radia ameiambia Mara Online News.

Kiwanda hicho zamani kilikuwa kinaitwa Mara Coffee Limited, kampuni ambayo ilikuwa ikinunua kahawa kwa wakulima katika wilaya ya Tarime na kusadia wakulima kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages