NEWS

Sunday 18 July 2021

Mbunge Kembaki atupa jiwe gizani upanuzi wa barabara Tarime Mjini




MBUNGE wa Tarime Mjini, Michael Kembaki (pichani juu) ametuma ujumbe mzito kwa mtu, au watu waliotaka kuweka msukumo wa kuruka kilomita sita wakati wa upanuzi wa barabara ya Nyamwaga kwa kiwango cha lami.

Akizungumza bila kumtaja mtu, katika mkutano wa hadhara mjini Tarime jana Julai 17, 2021, Kembaki amesema atasimama imara kuhakikisha barabara hiyo inapanuliwa kuanzia eneo la Jembe na Nyundo (Serengeti), bila kuhujumiwa.

“Tunahitaji barabara kwa maendeleo ya Tarime yetu, kuna kauli ilisemwa kwamba upanuzi wa barabara uanzie kule juu [eneo la Nyamwigura katika jimbo la Tarime Vijijini], naomba niwahakikishie, msimamo wangu na wa Serikali ni kwamba upanuzi utaanzia Jembe na Nyundo, ndio isonge kwenda kule, hapa haruki kitu,” amesisitiza Kembaki na kushangiliwa na umati mkubwa wa wananchi kuashiria kukubaliana na msimamo wa mbunge huyo.

Kembaki ametangaza msimamo wake huo - ikiwa zimepita siku chache baada ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, kuzungumza na wamiliki wa nyumba zinazotakiwa kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa wamiliki hao, David Mroni, Waitara waliwaelekeza kuwasilisha vielelezo vya ujenzi na umiliki wa nyumba hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, kwa hatua za ufumbuzi.

Maelekezo hayo yaliwafanya wamiliki hao kusitisha mpango wao kukimbilia mahakamani kuzuia utekelezaji wa notisi ya siku 30, inayowataka kubomoa nyumba zilizo ndani ya hifadhi ya barabara hiyo.

Barua ya notisi hiyo ilisainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Tarime, Erasto Mbunga ya Juni 30, 2021 ikieleza kuwa agizo hilo limetolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Nyamwaga kwa kiwango cha lami.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages