NEWS

Saturday 17 July 2021

Taasisi ya Kizalendo Tanzania yawasaidia wafungwa, wagonjwa TarimeMsaada gerezani

TAASISI ya Kizalendo Tanzania (TPO), leo Julai 17, 2021 imetembelea Gereza la Tarime na Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime na kugawa misaada mbalimbali kwa wahitaji.

Misaada iliyotolewa na TPO kwa wafungwa wa kike gerezani, wazazi na watoto waliolazwa hospitalini ni taulo za kike, sabuni za unga na miche za kufulia nguo.


Timu ya TPO iliyogawa misaada hiyo

Mwenyekiti wa TPO Wilaya ya Tarime, Philipo Lusotola amesema misaada hiyo imetokana na michango ya fedha kutoka kwa wanachama wa taasisi hiyo.

“Tumeona umuhimu wa sisi wanachama wa taasisi hii ya kizalendo kuja kuwaona ndugu zetu hawa na kuwafariji. Ninatoa wito kwa wananchi wengine kujenga moyo wa kizalendo wa kuja kusalimia na kusaidia ndugu zetu waliopo gerezani na hospitalini,” Lusotola amesema.

Lusotola akizungumza wakati wa kugawa msaada katika wodi ya watoto

Naye Mwenyekiti wa TPO Mkoa wa Mara, Dkt Emmanuel Obimbo amesisitiza umuhimu wa Watanzania kujenga utamaduni wa kutenga muda wao kwa ajili ya kutembelea na kusaidia wafungwa na wagonjwa.

“Unapokuwa mzalendo, unakuwa tayari kujitolea, hasa vijana ambao ndio taifa la leo na kesho, tuwe wazalendo kwa nchi yetu, tujitokeze pia kupima na kuchangia damu salama hospitalini,” Dkt Obimbo ameongeza.

Utoaji msaada ukiendelea wodi ya watoto

Kwa upande wao, Msaidizi wa Mkuu wa Gereza la Tarime, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Francis Makelemo na Mkuu wa kitengo cha wafungwa wanawake, Bernadeta Bwana wameishukuru TPO kwa moyo wa upendo na ukarimu waliouonesha kwa wafungwa hao.

“Msaada huu ni faraja kwetu, umeonesha mnatujali, endeleeni na moyo huu,” Makelemo amesema.

Ndani ya wodi ya watoto

Naye Muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Ghati Nyambanga ameishukuru TPO - akisema msaada huo wa sabuni utasaidia kuimarisha usafi wa nguo za wazazi na watoto waliozaliwa.

“Tunawashukuru TPO kututembelea na kutoa msaada huu, maana wazazi wengi huwa hawana mahitaji muhimu kama sabuni za kufulia nguo, lakini sasa watafua nguo zao - zitapendeza, na hata sisi wauguzi tutanawia mikono,” Muuguzi Ghati amesema.

Mazungumzo baina ya viongozi wa TPO na wauguzi katika wodi ya wazazi

Nao wazazi waliopata msaada huo, akiwemo Veronica Chacha, wameishukuru TPO kwa wema na moyo wa kujitolea kutoa msaada huo wa kibinadamu kwa watu wenye uhitaji, huku wakiiombea baraka kwa Mungu, izidi kufanikiwa na kusaidia wahitaji wengine katika jamii.

Kwa mujibu wa Mhazini wa TPO Mkoa wa Mara, James Nyakyoma, taasisi hiyo ya kizalendo ni zao la taasisi ya Magufuli Scholar Forum (MSF) iliyoanzishwa mwaka 2017.

Picha ya pamoja hospitalini

“Tumebadili jina la taasisi hii kutoka MSF kwenda TPO (Tanzania Patriotic Organisation) hivi karibuni, baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli,” Nyakyoma amefafanua.

Amesema lengo la TPO ni kuenzi mema yaliyofanywa na viongozi waasisi na wastaafu wa Taifa la Tanzania, lakini pia waliopo madarakani na kuhamasisha uzalendo, hasa kwa vijana kujitambua, kupenda, kuthamini, kulinda na kutetea maliasili na tunu za Taifa.

“Ndio maana pia kwa sasa tunashirikiana na wadau wengine kuhamasisha safari ya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa wakazi wa Tarime, itakayofanyika Julai 25, 2021,” Mwenyekiti wa TPO Wilaya ya Tarime, Lusotola ameongeza.


Nchi Yetu, Rais Wetu, Fahari Yetu

Viongozi na wanachama wengine wa TPO walioshiriki ziara hiyo ya kugawa misaada katika Gereza la Tarime na Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ni Martin Ngongi (Katibu Wilaya ya Tarime) na Ibrahim Mazubezi (Katibu Mkoa wa Mara).

Wengine ni Mwalimu Josheph Matiko (Afisa Miradi wa TPO Mkoa wa Mara), Mwalimu Teresia Sinyago (Mhasibu Wilaya ya Tarime), Thobias Jackson na Prisca Marwa (Wanachama wa TPO Wilaya ya Tarime). Kaulimbiu ya TPO inasema "Nchi Yetu, Rais Wetu, Fahari Yetu".

(Habari na picha zote: Christopher Gamaina wa Mara Online News)

1 comment:

  1. Hongereni sana TPO Tarime kwa kazi nzuri mliyoifanya

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages