NEWS

Tuesday 6 July 2021

Ustawi wa Bonde la Mto Nile: TNDF yakutunaisha wanachama, wadau Mwanza
UKWAA la Asasi za Kiraia katika Bonde la Mto Nile upande wa Tanzania (TNDF) limekutanisha wanachama na wadau wake jijini Mwanza, kuweka mkakati wa kusimimia utunzaji wa bonde hilo.

“Lengo la mkutano huu ni kubadilishana mawazo na kuweka mkakati wa pamoja, kwa ajili ya uhifadhi na usimamizi wa maji na rasilimali nyingine zote zilizopo katika bonde la mto Nile,” Mwenyekiti wa TNDF (Tanzania Nile Basin Discourse Forum), Donald Kasongi ameiambia Mara Online News katika mkutano huo unaoendelea kwenye ukumbi wa Adden Palace Hotel jijini Mwanza.Washiriki wa mkutano huo wanajadili mpango mkakati wa TNDF wa mwaka 2018 -2022, ambao pamoja na mambo mengine, unaweka msisitizo katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi katika vyanzo vya maji na diplomasia ya maji.

Pia ajenda ya madhara ya Covid-19 imejadiliwa katika mkutano huo muhimu wa wadau wa bonde la mto Nile upande wa Tanzania.

Aidha, Mratibu wa TNDF, Hadija Malimusi amesema mkutano huo ni fursa ya kuongeza ufahamu, uzoefu na kuangazia usalama wa chakula changamoto, mafanikio yetu na maendeleo ya jukwaa hilo kwa ujumla.Washiriki wa mkutano huo wametoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita na Simiyu.

Kasongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jukwaa la Asasi za Kiraia Bonde la Mto Nile (Nile Basin Discourse Forum) lenye asasi zaidi ya 600 katika mataifa 10 ikiwemo Tanzania, amasema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni kupungua kwa maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.

“Hivyo mkazo wetu ni kushughulika na mabadiliko ya tabianchi, hususan kwenye rasilimali za maji,” amesisitiza Kasongi.

Ameongeza kuwa mbali na uhifadhi, majukwaa ya NDF katika mataifa yote 10 yanatazama umuhimu wa ustawi wa maisha ya mamilioni ya watu katika bonde la Mto Nile.Kwa mujibu wa Kasongi, watalaamu wanaonya kuwa endapo hali itaachwa kuendelea ilivyo sasa, kuna hatari kwa baadhi ya maeneo ya dunia kukumbwa na vita ya maji kama ilivyokuwa katika suala la vita ya mafuta.

NDF ambayo makao makuu yake yapo Entenbe nchini Uganda, inafanya kazi kwa karibu na seriklai za mataifa 10 ambayo ni Tanzania, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, DR Congo, Egypt, Ethiopia na Sudan Kusini kupitia Nile Basin Initiative (NBL).

Hata hivyo, nchi ya Eritrea bado imebaki kuwa mtazamaji badala ya kuungana na mataifa mengine hayo yanayozunguka bonde la Mto Nile.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages