NEWS

Thursday, 8 January 2026

Tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29 yatua Mara, RC Mtambi aipokea



Mkuu wa Mkoa, Kanali Evans Mtambi, akiwaongoza Wajumbe wa Tume ya kuchungza matukio ya Oktoba 29 kwenda ofisini kwake, mara baada ya kuwapokea mjini Musoma leo.

Na Christopher Gamaina
akiripoti kutoka
Mara
---------

Wajumbe wawili wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Oktoba 29, 2025 wamewasili mkoani Mara na kupokewa na Mkuu wa Mkoa (RC), Kanali Evans Mtambi.

Wajumbe hao; Balozi Radhia Naima Msuya na Balozi David Joseph Kapya, wamepokewa na RC Mtambi mjini Musoma leo Alhamisi, Januari 8, 2026.

“Tumekuja tukiwa sehemu ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio baada ya uchaguzi na siku zilizofuata. Kulitokea kadhia ambayo ilipelekea watu kupoteza maisha, mali kuteketea.

“Mhe. Rais kwa mujibu wa sheria ameunda hii Tume ili kuchunguza kitu gani kimetokea, madhara gani yamepatikana, tunatokaje hapa,” Balozi Radhia amemueleza RC Mtambi.

“Tumefanya kazi Dar es Salaam – tumekutana na wadau mbalimbali, lakini tukapanga tuje na mikoani, hasa ile mikoa iliyoathirika na ile kadhia,” amesema Balozi Radhia na kuendelea:

“Kwa hivyo, tukagawanyika makundi matatu; wengine wameenda Kilimanjaro na Arusha, wengine Mbeya na Songwe na wengine ndiyo tulikuja hii kanda, tulikuwa Mwanza kwa siku tatu wanne, lakini tena tumegawanyika vikundi viwili; sasa wawili wameenda Geita, wawili ndiyo sisi tumekuja Mara.”


RC Mtambi (kulia) akiwa na wajumbe hao wa Tume ya uchunguzi ofisini kwake

Balozi Radhia amebainisha kuwa kesho Ijumaa, Januari 9 watakwenda wilayani Tarime, na kesho kutwa, Jumamosi 10 watakuwa wilayani Bunda kufanya kazi hiyo ya uchunguzi.

“Tumekuja kwa madhumuni hayo ya kujua kilitokea nini, tumepata athari gani na tunakwendaje huko tunakoelekea,” Balozi Radhia amesisitiza zaidi.

Naye Balozi Kapya amefafanua kwamba watasikiliza uongozi na timu ya mkoa pamoja na wadau mbalimbali ili kujua vitendo vilivyotokea na namna vilivyodhibitiwa.

“Tutawasikiliza - hii hali imekuwakuwaje, mliidhibiti namna gani, maanake Musoma ilisikika sana… tusikilize kwa makini na ushauri wenu. Mhe. Rais anataka kuona tunatoka hapa,” Balozi Kapya amemueleza RC Mtambi.

Kwa upande wake RC Mtambi amewakaribisha wajumbe hao wa Tume kufanya kazi yao kwa uhuru mkoani Mara.

“Tuna matumaini makubwa na Tume, tunawakaribisha sana mfanye kazi hii iliyotukuka ili mtusaidie kama mkoa, lakini pia kama taifa. Hatutaki turudi tena kwenye hali hiyo,” RC Mtambi amewambia wajumbe hao wa Tume.

Tume hiyo ya uchunguzi ina jumla ya makamishna/ wajumbe tisa, na ilipewa siku 90 kufanya kazi hiyo.

Mbali na Balozi Radhia Naima Msuya na Balozi David Joseph Kapya, wajumbe wengine ni Dkt. Stergomena Tax, Prof. Ibrahim Hamis Juma, Balozi Ombeni Yohana Sefue, Said Ally Mwema, Balozi Paul Meela, Balozi George Kahema Madafa na Jaji Mohamed Chande Othman ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliunda tume hiyo kuchunguza vurugu zilizosababisha vifo na majeruhi kwa watu, uharibifu wa mali za uma na watu binafsi kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2026 katika majiji na miji mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages